KUKUTANA KIMWILI KABLA YA NDOA NI CHANZO KIKUU CHA CHUKI.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

◼️Dhambi ya uasherati ambao hufanywa na wachumba kabla ya Ndoa Ina madhara mengi, ndio maana Biblia inasema Kila Mtu aikimbie zinaa yaani aikimbie kufanya mapenzi na Mtu yeyote asiye mwenzi wake waliooana.
 
1 Wakorintho 6:18 "Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe."

◼️Baadhi ni madhara ya kukutana kimwili kabla ya Ndoa ni kuchukiana.

➡️Mfano hai ni huu

2 Samweli 13:11-20 " Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako.
 Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza. Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake. Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake. Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti. Huyo Absalomu nduguye akamwambia, je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili. Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa nyumbani mwa nduguye Absalomu."

➡️Binti huyu alikuwa Bikra, watu wote wanafahamu thamani ya Mtu kuwa bikra lakini ilipowezekana tu kukutana na Kijana kimwili Bikra haikuzuia kuchukiwa, Bikra haikuwa kitu Tena maana tendo la uzinzi ni dhambi iliyomleta shetani kwenye mioyo yao.

◼️Neno hili likuamshe Kijana au Binti ambaye kweli unaitarajia Ndoa njema.

◼️Kitendo Cha kukutana kimwili kabla ya Ndoa kinaweza kuifuta Ndoa na kitendo hicho kikapanda chuki .

➡️Kwa Binti Tamari ilipowezekana tu kukutanana kimwili na Kijana Amnoni Kila kitu Cha kimahusiano kilibadilika hata kama haikuwa kwa ridhaa yake.

◼️Yaliyotokea baada ya kukutana kimwili kabla ya Ndoa ni haya.

1.  Kijana ghafla tu akamchukia Binti kwa machukio makuu baada ya kulala naye kingono.

"Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; " 

➡️Kabla hajazini naye alikuwa anampenda sana na anavutiwa naye sana lakini baada tu ya kuzini naye akamchukia machukio makuu.

➡️Binti hata kwako inaweza ikatokea ukiruhusu uasherati na Mchumba wako.

2. Upendo wa kwanza ukaondoka ikaja chuki, shetani amepanda magugu.

"kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza."

➡️Leo ni watu wengi sana uchumba wao upo kama haupo au uchumba wao una migogoro mingi na muda wowote uchumba huo unavunjika, chanzo Cha migogoro yote ni chuki iliyotengenezwa na kukutana kimwili kabla ya Ndoa.

3. Binti akafukuzwa.

"Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako."

◼️Binti au Kijana elewa jambo hili kwamba ni rahisi sana kuachana baada ya kuanza kukutana kimwili kabla ya Ndoa.

➡️Ni rahisi mno Kijana kumwandikia Binti kama hivi "Kuanzia Leo Mimi na Wewe basi, nimempata aliye Bora kuliko Wewe"

Je ubora wako uliisha lini?
Ubora wako uliisha siku ulipokubali tu kulala naye kimwili.

4. Mlango wa uhusiano hufungwa.

"Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake."

 ◼️Ni Vijana wengi sana na wachumba wengi sana ambao mlango wa Kufunga Ndoa na wachumba wao ulifungwa baada tu ya kuzini nao.

◼️Ujumbe huu ni wa onyo kwako Wewe Kijana au Binti unayetamani Ndoa, uasherati utafunga mlango wa Ndoa kwako hivyo tubu na Anza upya na Bwana YESU KRISTO ili akusamehe na kukupa Neema mpya ili ukipata Mchumba Tena usikosee.

5. Maumivu na vilio vikaambatana na Binti.

"akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti."

➡️Vipi unaachwa kipindi Kijana huo au Binti huyo unampenda sana?

Sababu ni kama tu  utaruhusu kukutana kimwili kabla ya Ndoa, ukifanya hivyo lazima mmoja wenu ndani yake iingie roho ya kutaka kuachana.

◼️Ndio maana huwa Kuna ugumu sana kwa wachumba waasherati katika suala la Kufunga Ndoa.

6. Binti kukaa hali ya Ukiwa.

"Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa"

➡️Ukiachwa lazima utabaki na Ukiwa na unaweza hata kupata madhara ya kimwili.

 ◼️Chanzo ni kukutana kimwili kabla ya Ndoa, jitunze na zingatia sana kutokumpa Mchumba wako nafasi ya kukutana kimwili na Wewe kabla ya Ndoa kama kweli unaihitaji Ndoa Takatifu.

7. Kijana kuchukiwa na kupelekea kifo chake.

2 Samweli 13:28 "Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, ndipo mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, iweni na ujasiri."

➡️Hii ndio mbaya zaidi yaani uasherati uliikaribisha roho ya mauti kwako na ikampata.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments