MAOMBI YA KUBOMOA MADHABAHU ZA GIZA, MTU MMOJA AMEIBOMOA MADHABAHU ILIYOKUWA INATEGEMEWA NA MJI WOTE.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU Kisha tuombe Maombi ya ushindi Mkuu.


◼️Ukisoma Waamuzi 6:12 unaona Gideoni kwenye ulimwengu wa roho alikuwa anaonekana shujaa ndio maana Malaika akamwita shujaa, Biblia inasema hivi "Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia, BWANA yu pamoja nawe, Ee shujaa."


➡️Lakini katika ulimwengu wa mwili Gideoni na wenzake walikuwa Wanyonge wanaoonewa na Wamidiani.


Waamuzi 6:13 "Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani."


◼️Ushujaa wa Gideoni ulikuwa haujawahi kuonekana kwa sababu ya madhabahu ya giza iliyokuwa nyumbani kwao.


➡️Na madhabahu hiyo ya giza hii ilikuwa madhabahu ya familia kwa sababu ilikuwa Nyumbani kwa akina Gideoni.


➡️Madhabahu ya giza pia ilikuwa madhabahu ya Ukoo kwa sababu  ilikuwa Nyumbani kwao na Baba yake ndio Kiongozi wa Ukoo wako.


➡️Madhabahu hii ya giza pia ilikuwa madhabahu ya mji ndio maana Watu wa mji ndio waliotaka kumpiga Gideoni baada ya kuibomoa.


◼️Hadi hapo ushujaa wa Gideoni uliosemwa na Malaika haukuwahi kufanya kazi.


◼️◼️Ndipo  MUNGU Akamwambia achukue Sadaka  aivunje madhabahu hiyo ya shetani iliyokuwa unafanya kazi kwenye familia, Ukoo na mji.


Waamuzi 6:25" Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo;"


◼️◼️Maajabu ni kwamba Mtu mmoja tu kwa sadaka ameiangusha madhabahu ya giza ya Ukoo na mji.


Waamuzi 6:31 "Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake."


◼️◼️Baada ya kuibomoa madhabahu hiyo ya giza tunamuona Gideoni ushujaa wake ulioonwa na Malaika, huo ushujaa ukaanza kujidhihilisha katika Maisha yake.


➡️Kwanza ROHO MTAKATIFU akawa juu yake, hofu ikaondoka.


Waamuzi 6:34" Lakini roho ya BWANA ikaja juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata."


➡️Baada ya kuibomoa madhabahu ya giza na ushujaa wake kurudi  Wamidiani hadi ndoto tu zilianza kuwatisha wakajikuta wanajikabidhi kushindwa mbele ya Gideoni bila hata vita kuanza.


Waamuzi 7:13-14 " Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake."


➡️Baada ya kuangusha madhabahu ya giza ushujaa wa Gideoni ukaanza kuonekana.


Waamuzi 7:9 "Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako."


➡️Baada ya madhabahu ya giza kuangushwa ushujaa wa Gideoni ulianza kuonekana.


Waamuzi 7:21" Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza."


 ◼️Ndugu, Kuna Maisha ya ushindi Kila eneo la Maisha Yako kama ukiibomoa  na kuiangusha madhabahu ya giza iliyokufunga.


Kumbu 12:3 "nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo."


◼️MUNGU siku zote anataka uvunje madhabahu za giza zinazokutesa.


Hosea 10:2 "Moyo wao umegawanyika; sasa wataonekana kuwa na hatia; yeye atazipiga madhabahu zao, ataziharibu nguzo zao."


◼️Rafiki mpendwa omba na utamuona MUNGU wa Mbinguni katika Maisha Yako.


➡️Mambo Yako yaliyosimama baada ya kuivunja madhabahu ya giza na kuisimamisha madhabahu ya MUNGU, mambo Yako hayo yataanza upya katika ushindi.


◾Kanuni Muhimu sana za kufanya unapoombea kuondoa madhabahu ya giza katika Maisha Yako.


A. Ivunje na kuibomoa madhabahu hiyo ya giza.


B. Ndugu Hakikisha katika Maombi ya Leo unaibomoa na kuivunja madhabahu ya giza na baada ya kuiangusha weka Damu ya YESU KRISTO ili mawakala wa shetani wasifanikiwe Tena kuweka madhabahu yao hapo.


C. Baada ya Maombi Yako simamisha madhabahu ya MUNGU katika nyumba Yako, kazi Yako, familia Yako, Ukoo wako, mji uliopo, Kanisani n.k


Mwanzo 26:25 "Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko."


◾Je madhabahu ya giza inazuia Nini kwako?


◾Je madhabahu ya giza imezuia Ndoa au uzao?


◾Je madhabahu ya giza inazuia uchumi au maendeleo Yako.


◾Je madhabahu ya giza imeleta magonjwa kwako, mikosi na balaa zisizoisha?


◼️Ndugu katika Jina la YESU KRISTO Kuna kushinda na zaidi ya kushinda kwa yeye YESU KRISTO aliyetupenda.


Warumi 8:37 "Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda."


➡️Faida  za kuwa na madhabahu ya MUNGU ni nyingi mbili kati ya nyingi ni hizi.


1. Madhabahu ya MUNGU inaweza kuzungumza hivyo ukawa unashinda vita za kiroho bila kutumia Nguvu.


Ufunuo  16:7 "Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, BWANA Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako."


2. Malaika husimama pembeni ya madhabahu ya MUNGU, hivyo msaada wa MUNGU kwako ni hapo hapo.


Luka 1:11" Akatokewa na malaika wa BWANA, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia."


◼️◼️Ndugu vunja madhabahu za giza Kisha katika eneo hili isimamishe madhabahu ya MUNGU katika KRISTO YESU katika eneo hilo ili adui asisimamishe madhabahu nyingine eneo hilo.

Huo ndio ushauri wangu Mimi Peter Mabula kwako rafiki yangu unayejifunza somo langu hili ambalo MUNGU amenipa kwa Ajili Yako.


Nini ufanye katika Maombi?


1. Tubia dhambi zako zote na Uovu ili uwe safi mbele za MUNGU.


Yeremia 14:20 "Ee BWANA, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi."


2. Bomoa madhabahu za giza zilizokushikilia.


Kutoka 34:13 "Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao.''


3. Wapige mapigo watenda kazi wa Madhabahu hiyo ya giza.


Kumbu 12:3 "nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo."


4. Baada ya kuibomoa madhabahu ya giza achilia damu ya YESU KRISTO eneo hilo.


Ufunuo  12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."


5. Baada ya kuondoa madhabahu ya giza simamisha madhabahu ya kiroho ya YESU KRISTO katika eneo hilo.


1 Wafalme 18:30 "Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika."


6. Mshukuru MUNGU umeshinda.


Zaburi 52:9 "Nitakushukuru milele kwa maana umetenda; Nitalingojea jina lako kwa kuwa ni jema; Mbele ya wacha MUNGU wako."

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe

Comments