![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Kuomba au Maombi ni Nini?
➡️Kuomba ni kutaka kitu au msaada kutoka kwa MUNGU.
Zaburi 116:4 "Nikaliitia jina la BWANA. Ee BWANA, nakuomba sana, Uniokoe nafsi yangu."
➡️Maombi ni kupeleka mahitaji Yako kwa MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Yohana 16:24 'Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu."
◼️Kuamuru ni Nini?
➡️Kuamuru ni kutoa amri ili kupata kitu unachokitaka.
➡️Kuamuru ni kulazimisha Mwingine atende unavyotaka.
➡️Kuamuru ni kuagiza kutendeka unachotaka.
✔️✔️Katika Maombi Yako mbele za MUNGU zingatia vipengele hivyo viwili yaani "Kuomba" na "Kuamuru "
◼️Wewe Mwanadamu huwezi kumwamuru MUNGU lolote, unachoweza Wewe ni kumuomba yeye kwa unyenyekevu.
Mwanzo 24:12 "Naye akasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu."
➡️Ila katika Maombi kuamuru kupo na Kuna matokeo pia, hivyo Jifunze ili ujue unaamuru Nini.
◼️Mapepo ili yatoke unatakiwa uyaamuru kutoka na sio kuyaomba kutoka.
Marko 1:27 "Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!"
◼️Ukisoma Maandiko unaona Bwana YESU kuna wakati alikuwa anaomba kwa Baba yake.
Mfano hapa
Yohana 17:15 "Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu."
◼️Lakini pia Kuna wakati Bwana YESU alikuwa anaamuru na sio kuomba.
Marko 9:25 "Naye YESU akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena."
➡️Ndio maana tunajifunza Sasa ili tujue sehemu ya kuomba na sehemu ya kuamuru katika Maombi yetu.
◾Kwanini tuwe na Maombi ya kuamuru?
◼️Ni kwa sababu Mamlaka ya Jina la YESU KRISTO Iko ndani yetu na Bwana YESU anataka tuitumie.
Luka 21:15 ''kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga."
➡️Nini tuamuru katika Maombi yetu ya kuamuru Leo?
1. Amuru Nguvu za giza ziondoke katika eneo la Maisha Yako unayotaka ziondoke.
Marko 9:25 "Naye YESU akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena."
2. Kwa Mamlaka ya Jina la YESU KRISTO amuru baraka fulani unazozitaka ili zije kwako.
Kumbu 28:8" BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako."
3. Amuru maadui wako wa kiroho kuondoka katika eneo la Maisha Yako unalotaka waondoke.
Yoshua 23:10 "Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana BWANA, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia."
4. Kama Kunguru wanaweza kuamriwa na MUNGU wakulishe nini kinashindikana?
1 Wafalme 17:4 "Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko."
◼️Amuru watu waliobebeshwa na MUNGU baraka zako, amuru watokee kwenye Maisha Yako ili ufanikiwe.
5. Amuru vitu fulani visimame kwa kusudi maalumu kwa ajili ya ushindi wako.
Yoshua 10:12-13 " Ndipo Yoshua akanena na BWANA katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni. Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao."
➡️Huyu aliamuru jua na mwezi visimame vikasimama, hii una maana Wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU Wana wamlaka kubwa.
◼️Wewe simamisha uchawi unaofanyika kwa Watoto wako au familia Yako n.k
◼️Kwa Mamlaka ya Jina la YESU KRISTO simamisha kuibiwa katika biashara Yako n.k
6. Amuru kuhamisha milima ya matatizo kwenye Maisha Yako.
Mathayo 21:21 "YESU akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng'oka, ukatupwe baharini, litatendeka."
7. Mshukuru MUNGU amejibu Maombi Yako.
Wakolosai 4:2 "Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;"
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments