MUNGU ANAWEZA AKAPIGANA NA WANAOPIGANA NA WEWE.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.

◼️MUNGU anaweza akapiganana na wanaopigana na Wewe.

Mfano hai ni huu

Yoshua 10:42 "Na wafalme hao wote na nchi zao Yoshua akatwaa, wakati huo, kwa sababu yeye BWANA, Mungu wa Israeli, ALIPIGANA KWA AJILI YA ISRAELI,"

 ◼️Ndio maana tunaona baadhi ya Watumishi wa MUNGU wa Zamani wakiomba Maombi ya kumwambia MUNGU apigane na adui zao na alifanya hivyo.

Zaburi 35:1 "Ee BWANA, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami."

◼️Lakini pia huwa Kuna sababu hadi MUNGU apigane na adui zako kwa ajili Yako.

Hesabu 10:9 "Tena hapo mtakapokwenda kupiga vita katika nchi yenu, kupigana na adui awaoneaye ninyi, ndipo mtakapopiga sauti ya kugutusha kwa tarumbeta; nanyi mtakumbukwa mbele za BWANA, Mungu wenu, nanyi mtaokolewa na adui zenu."

◼️Sababu 7 zinazoweza kumfanya MUNGU apigane na adui zako kwa ajili yako Mteule wa KRISTO.

1. MUNGU anaweza akapigana na adui zako kama unaishi katika kusudi lake na unafanya kazi yake.

1 Samweli 7:10 "Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini BWANA akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli."

◼️Samweli alikuwa anaishi katika kusudi la MUNGU hivyo kupiganiwa na MUNGU ilikuwa rahisi sana.

Tunaona katika andiko hili Samweli alikuwa akifanya kazi ya MUNGU kipindi wanavamiwa, yeye akaendelea na kazi hiyo ya MUNGU na MUNGU akawapiganiwa wao.

◼️Kuna mazingira MUNGU atapigana na adui zako kwa sababu tu Wewe unaishi katika kusudi lake na unamtumikia kwa uaminifu katika KRISTO YESU.


2. MUNGU anaweza akapigana na adui zako kama umeomba apigane nao.

2  Nyakati 20:1-4 " Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani. Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng'ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi). Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute BWANA; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta BWANA."

◼️Katika maandiko haya tunaona Watu wa Israeli waliamua Kumtafuta MUNGU Kwa Maombi na Maombi ya Kufunga, hivyo MUNGU akapigana na adui zao walikuwa na Nguvu sana ambao walikuwa ni mataifa matatu yaliyokuja kupigana na Taifa Moja ambalo ni Israel.

2  Nyakati 20:14-14 "Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya MUNGU."

◼️Hapa tunajifunza kwamba vita ilikuwa yao kabla hawajaanza Maombi, ila walipoanza Maombi vita ikawa ya MUNGU na wakashinda, MUNGU aliinunua vita yao kupitia Maombi yao.

➡️MUNGU alipigana na adui za Israeli kwa sababu tu Waisraeli waliomba MUNGU awashindie.

◼️Hata kwako Bwana YESU KRISTO anaweza akapigana na adui zako Wachawi, mizimu na Wanadamu wabaya kwa sababu tu umeomba hivyo.

➡️Hapo ndipo tunaona Nguvu za Maombi, Ndugu usiache kuomba Maombi Mfano Maombi ya ulinzi kwako na Kwa familia Yako.

3. MUNGU anaweza akapigana na adui zako pale anapotaka adhihilishe Nguvu zake.

1 Samweli 17:45-50 " Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, MUNGU wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko MUNGU katika Israeli.
Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti.
 Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake."

◼️Katika maandiko hapo Daudi anasema " Ili Dunia nzima wajue Yuko MUNGU katika Israeli " maana yake MUNGU alimpiga Goliathi na Wafilisti wanaotisha na wenye Nguvu sana ili ulimwengu wote ujue kwamba Yuko MUNGU anayeweza kuwapigania watu wake.

➡️MUNGU alipigana na Goliathi kupitia Daudi ili azidhihilishe Nguvu zake.

◼️Hata kwako MUNGU anaweza akapigana na watu wabaya na mawakala wa shetani wa Kila namna ili azidhihilishe Nguvu zake, watu wote wajue Wewe uko na YESU KRISTO Mwokozi.

4. MUNGU anaweza akapigana na adui zako kama Wewe umemfanya yeye kuwa Mkombozi wako Pekee na Unaomba.

Isaya 41:10-14 " usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia. Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema BWANA, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli."

◼️MUNGU katika maandiko haya anasema atamsaidia Yakobo kwa sababu yeye MUNGU ni Mkombozi wa Yakobo.
Hadi MUNGU anasema Yeye ni Mkombozi wa Yakobo ujue Yakobo ndio aliamua kuchagua MUNGU awe Mkombozi wake.

➡️MUNGU alipigana na adui za Yakobo kwa sababu Yakobo alimfanya MUNGU wa Mbinguni kuwa Mkombozi wake.

◼️Hata wewe Bwana YESU KRISTO anaweza akapigana na adui zako kiroho kwa sababu umemfanya kuwa Mwokozi na Mkombozi wako, Fanya hivyo ukihitaji MUNGU apigane na adui zako wote.

5. MUNGU anaweza akapigana na adui zako kama Wewe unatembea katika Mapenzi yake.

Yeremia 1:19 "Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe."

◼️MUNGU hatapigana tu na adui zako Bali atapigana na adui zako kwa sababu Wewe unaishi katika mapenzi yake.

➡️Kutembea kwenye mapenzi ya MUNGU ni kufanyaje?

◼️Kutembea kwenye mapenzi ya MUNGU ni kwamba atakacho MUNGU ndio na Wewe unakitaka na utatembea katika hicho.

◼️Kutembea katika mapenzi ya MUNGU ni matakwa ya MUNGU wa Mbinguni na matakwa Yako yanaambatana na kuwa kitu kimoja.

◼️Mapenzi ya MUNGU Maana yake nyingine ni unachopenda Wewe na anachopenda MUNGU kiwe kitu kimoja, anachopanga MUNGU katika KRISTO YESU na unachopanga Wewe kiwe kitu kimoja, unachotenda kiwe ni kile anachotaka MUNGU daima.

◼️Njia kuu kuliko zote ya Wewe kutembea kwenye mapenzi ya MUNGU ni Wewe kuishi na Kuenenda katika ROHO MTAKATIFU kwa kufuata tu kile ROHO MTAKATIFU anataka.

◼️Sasa Ukiwa unaishi katika mapenzi ya MUNGU uwe na uhakika kwamba Kuna vita ya kiroho MUNGU atapigana na adui zako kwa sababu hiyo tu na Wewe ndio utashinda.

6. MUNGU anaweza akapigana na adui zako na Kwa njia ya kukulinda kama Wewe huwa unasaidia wahitaji na Wanyonge.

Zaburi 41:1-2 " Heri amkumbukaye mnyonge; BWANA atamwokoa siku ya taabu. BWANA atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake."

◼️MUNGU huwa ana tabia ya kuwalinda watu wale wanaosaidia Wahitaji na Wanyonge na wahitaji.

◼️Njia mojawapo ya MUNGU kuwalinda ni kupigana na adui zao, hivyo ukiwa na tabia ya kudumu ya Kusaidia Wanyonge na wahitaji MUNGU atapigana na adui zako ili akulinde, Kumbuka MUNGU huangalia Neno lake ili alitimize.
Yeremia 1:12 "Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana NINALIANGALIA NENO LANGU, ILI NILITIMIZE."

◼️Wanyonge na wahitaji ni kama Yatima, Wajane, wazee wasiojiweza, Walemavu wasiojiweza, Wagonjwa wasiojiweza n.k
Ukiwasaidia hawa umesaidia Wanyonge, ipo siku MUNGU atakulinda kwa sababu Wewe una tabia ya Kusaidia Wanyonge.

◼️Wahitaji ni kama Wahubiri ambao unatoa pesa zako ili waenda kuhubiri Injili, hizo nauli au uwezeshaji unaoufanya utamfanya MUNGU akulinde sana.

◼️Namna nyingine ya Kusaidia Wanyonge ni hii, Usione Mtu anaonewa na Wewe ukaacha kumsaidia ingawa una uwezo wa kumsaidia, Mfano Wewe ni wakili na Yuko mama unamfahamua anataka kudhulumiwa Mali zake na Ndugu wa Mume wake baada ya Mumewe kufariki na kesi ipo mahakamani, ukimsaidia umesaidia Wanyonge na MUNGU atakulinda kwa sababu ya Kusaidia Wanyonge huu ni Mfano mmoja kati ya MUNGU ya namna unavyoweza Kusaidia Wanyonge na MUNGU atakulinda sana.

7. MUNGU anaweza akapigana na adui zako kwa kukulinda kama ni yeye amekuweka sehemu kwa kusudi lake na Wewe unaishi katika mapenzi yake katika KRISTO YESU.

Yeremia 15:20 "Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema BWANA."

◼️MUNGU kama amekuweka eneo fulani na unatumiza Wajibu wako atakulinda, na njia mojawapo ya kukulinda ni kupigana na adui zako ili wasikuguse uendelee kufanya kazi ya MUNGU katika KRISTO YESU.

➡️Mfano MUNGU amekuweka kuwa Mchungaji, Mhubiri, Askofu, Mwimbaji Kanisani, Kiongozi wa Vijana, Kiongozi wa Wanawake, Mwalimu wa Watoto, unayewategemeza Watumishi kwa pesa zako, unalinda Kanisa, ni Mwana Maombi Kanisani n.k
Kama MUNGU ni MUNGU amekuweka katika utumishi huo na unautimiza atakavyo MUNGU uwe na uhakika atakulinda na atapigana na adui zako kwa ajili Yako ili uendelee kumtumikia yeye katika KRISTO YESU Mwokozi.

◼️◼️Ndugu katika Maisha Yako Tafuta nafasi ya MUNGU kupigana na adui zako kwa ajili Yako.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments