MUNGU ANAWEZA KUTHIBITISHA MTU KWAKO.


Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

◼️Wakati Mwingine macho ya kibinadamu hayawezi kuona vyema kama inavyotakiwa.

◼️Wakati Mwingine Mwanadamu ukitegemea akili zako huwezi kuamua vyema kulingana na ulichoona.
Ni MUNGU tu ndio anayejua Siri ya Moyo wa Mtu na anaweza kuuchunguza Moyo wa Mtu na kujua kilichopo.

Zaburi 44:21 "Je! MUNGU hatalichunguza neno hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo."

➡️Kuna watu wengi tunatamani Kushirikiana nao lakini sio watu wazuri kwetu.
Ni vizuri sana kumshirikisha MUNGU katika ROHO MTAKATIFU maana ni yeye tu anayeweza kulipima jambo ndani ya moyo wa Mtu na akakupa majibu Sahihi.

1 Samweli 2:3 "Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani."

➡️Unaweza ukachagua kutokufuata ushauri wa Bwana YESU KRISTO lakini lazima ukutane na madhara, hivyo ni vizuri mno Kumsikiliza Yeye ndio mwenye majibu Sahihi ya mambo mbalimbali ya Maisha Yako.

Yoshua 9:14 "Basi hao watu wakatwaa katika vyakula vyao, wala wasitake shauri kinywani mwa BWANA."

◼️Moyo wa Mwanadamu ni kichaka kizito sana hivyo unamhitaji sana ROHO MTAKATIFU ili ufanye maamuzi sahihi juu ya nani wa Kushirikiana nae au kuambatana nae.

Mimi Peter Mabula Nipo hapa Leo kukuambia kwamba MUNGU anaweza kukujulisha juu ya Mtu Fulani kwa ajili ya Kushirikiana nae au kwa ajili ya kusudi la MUNGU.

1 Samweli 9:17 "Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu."

◼️Kama Wanadamu wakati Mwingine ni rahisi kukosea kuchagua watu wa kuambatana nao kwa sababu tumeangalia kimwili au kibinadamu, ni macho ya MUNGU tu ndio yanayoweza kumuona Mtu kwa usahihi.

◼️ROHO MTAKATIFU anaweza kumtazama Mtu hadi miaka 50 ijayo atakuwaje, huyo ndio wa kumshirikisha Ukitaka ufanikiwe bila matatizo.

◼️Macho ya kibinadamu hutazama kibinadamu hivyo ni Muhimu sana kumhitaji MUNGU kuhusu maamuzi yetu.

Neno la MUNGU linasema mambo yote tunafanyayo au tunayokusudia kuyaamua ni vyema sana tukayafanya katika Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

➡️Siku Moja Samweli alidhani Eliabu ndio atakuwa Mfalme wa Israeli MUNGU Akamwambia sio yeye.

1 Samweli 16:6-7 " Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo."

➡️Alipokuja Abinadabu Samweli kwa macho ya kiroho alisema "Huyo hakuchaguliwa na MUNGU"

1 Samweli 16:8 "Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, BWANA hakumchagua huyu."

◼️◼️Hiyo yote inatufundisha kwamba ni Muhimu sana kumshirikisha MUNGU katika mipango yetu na maamuzi yetu pale tunapotaka kushirikiana na Watu.

Mfano hii inatufundisha kwamba;

1. MUNGU anaweza kukusaidia kukuchagulia Mtu sahihi wa kufanya nae kazi au kumpa jukumu.

Waamuzi 1:1-2 " Ikawa baada ya kufa kwake Yoshua, wana wa Israeli wakamwuliza BWANA, wakisema, Ni nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu juu ya Wakanaani, ili kupigana nao? BWANA akasema, Yuda atakwea; tazama, nimeitia hiyo nchi mkononi mwake."

◼️MUNGU aliwasaidia Waisraeli kumchagua Yuda kwa ajili ya kushinda vita na wakashinda baada ya kufanya uchaguzi sahihi.

2. Mtu sahihi ni yule anayechaguliwa na MUNGU sio yule Mtu anajichagulia.

1 Samweli 16:12" Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. BWANA akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye."

◼️Daudi alikuwa baraka kwa wengi na alifanya mambo makubwa kuliko Wafalme wote wa Israeli kwa sababu alichaguliwa na MUNGU.

Mtu aliyechaguliwa na MUNGU ni baraka kwa wengi.
Hata leo Bendera ya Israel ina alama ya ishara ya Daudi.

3. Mtu Bora kwenye macho ya watu anaweza asiwe aliyechaguliwa na MUNGU wa Mbinguni.

1 Samweli 16:7 "Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo."

◼️Samweli kidogo akosee kuchagua Mtu sahihi hadi MUNGU akamrekebisha, hivyo tunafundishwa kwamba Mtu sahihi katika macho ya kibinadamu anaweza asiwe Mtu sahihi kwa MUNGU wa Mbinguni.

4. Kuna madhara kufanya kazi na Mtu asiyetokana na MUNGU wa Mbinguni.

1 Wafalme 16:31 "Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia."

◼️Ahabu alipomuoa tu Yezebeli ndio anguko lake likaanza na likawa baya kwake hadi kwa taifa, hii ilipelekea hadi alipokufa watu wakakataa kumzika katika makaburi ya Wafalme.

➡️Ndugu, Inawezekana unahitaji Mtu wa Kushirikiana nae kwenye biashara.

➡️Inawezekana unahitaji Mtu wa Kufunga naye Ndoa.

◼️Ndugu Jifunze tabia ya kuuliza kwa MUNGU kwanza kupitia ROHO MTAKATIFU.

Nini ufanye kama ulikosea katika kuchagua?

1. Tubia maamuzi ya akili yako  yaliyochagua  kinyume na kusudi la MUNGU.

Mithali 3:5" Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;"

2. Uliza kwa MUNGU ni nani Mtu sahihi au ni nani atakuwa msaada kwako katika uchaguzi mpya utakaoufanya wa marafiki wa Kushirikiana nao.

Waamuzi 20:18 "Basi wana wa Israeli wakainuka, wakakwea kwenda Betheli, nao wakataka shauri kwa MUNGU; wakasema, Ni nani atakayekwea kwenda vitani kwanza kwa ajili yetu juu ya wana wa Benyamini? BWANA akawaambia, Yuda atakwea kwanza."

◼️Kumbuka kama ulikosea kuhusu mwenzi wa Ndoa na ukafunga nae Ndoa, hapo huhitaji kuuliza kwa MUNGU Bali muombee mwenzi wako awe kama MUNGU atakavyo maana Agano la Ndoa ni Agano kubwa ambalo hairuhusiwi kulivunja, ukiingia umeingia hivyo hakuna option ya kusema uombe upya ili kupewa, lakini Mchumba unaweza ukauliza na hata ukavunja Ukitaka ila sio Ndoa.

Ila kama ni marafiki au wakufanya nao kazi unaweza kuuliza kwa MUNGU lakini sio Ndoa ambayo uko ndani yake.

3. Fuata maelekezo ya MUNGU anapokuambia juu ya Mtu Fulani hata kama mtazamo wako Wewe juu ya Mtu huyo unakataa.

Mathayo 1:20 "Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa BWANA alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa ROHO MTAKATIFU."

◼️Kumbuka MUNGU hakosei na hajawahi kukosea katika kukuchagulia hivyo fuata maelekezo ya MUNGU hata kama unaona yanakuumiza.

4. Ishi Maisha ya kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.

Wagalatia 5:25 "Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO."

Ukikubali kuongozwa na ROHO MTAKATIFU hutakwama popote pale iwe katika uchaguzi wa marafiki maana ROHO MTAKATIFU atakuwa pamoja na Wewe na kukushauri uamuzi sahihi.

Zaburi 32:8-9 " Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama. Msiwe kama farasi wala nyumbu, Walio hawana akili. Kwa matandiko ya lijamu na hatamu Sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia."

5. Hakikisha unakuwa Mtu wa kuuliza kwa MUNGU katika maamuzi magumu ya Maisha Yako Mfano Kuoa, kuolewa n.k

Mwanzo 24:42-45 " Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi, tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe, naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia zako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke BWANA aliyemwekea mwana wa bwana wangu. Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe."

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments