![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Kuna Nguvu kubwa katika kuona.
Mfano umeona Ndotoni kwamba kitu fulani kitakuwa hivi kwako baada ya muda fulani, utatiwa Nguvu hata watu wakikukatia tamaa utawashangaa tu kwa uliona hivyo una uhakika na ulipata Nguvu ya kuendelea baada ya kuona.
➡️Yakobo alikuwa ameona kwenye ulimwenguni wa roho juu ya Ephraim na Manase ambao ni Watoto wa Yusufu.
Nguvu ya kuona ilimfanya Yakobo wakati wa kubariki Watoto wale afanye kama alivyoona ingawa Yusufu alidhani anakosea.
Mwanzo 48:17-19" Yusufu alipoona kwamba babaye anaweka mkono wake wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, ikawa vibaya machoni pake. Akauinua mkono wa babaye auondoe katika kichwa cha Efraimu, ili auweke juu ya kichwa cha Manase. Yusufu akamwambia babaye, Sivyo, babangu, maana huyu ni mzaliwa wa kwanza; weka mkono wako wa kuume kichwani pake. Babaye akakataa, akasema, Najua, mwanangu najua, yeye naye atakuwa taifa, yeye naye atakuwa mkuu; lakini ndugu yake mdogo atakuwa mkubwa kuliko yeye, na uzao wake watakuwa wingi wa mataifa."
◾Yakobo alikuwa ameona kwenye ulimwenguni wa roho ndio maana akalijua kusudi la MUNGU juu ya watoto wale, kusudi la MUNGU Kwa Watoto wale lilikuwa tofauti kabisa na taratibu za kibinadamu, Yusufu akataka taratibu za kibinadamu ndio zifanyike kwa sababu alikuwa hajaona katika ulimwengu wa roho, Yakobo kwa sababu alikuwa ameona kwenye ulimwenguni wa roho haikumsumbua hivyo akatekeleza kama kusudi la MUNGU lilivyo juu ya watoto wale, hiyo ndio Nguvu ya kuona.
◼️Mifano zaidi ya Nguvu ya kuona ni hii;
1. Nguvu ya kuona iliwafanya Wafilisti wakimbie baada ya kuona Goliathi mkuu wao amekufa mbele ya Kijana Mdogo aitwaye Daudi.
1 Samweli 17:51 "Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia."
➡️Wafilisti wasingeona Goliathi amekufa wasingekimbia, Nguvu ya kuona Matendo ya MUNGU inaweza kuwafanya adui zako wakimbie na kuyaachia Maisha Yako.
◼️Nguvu ya kuona ikawafanya Wafilisti wakimbie.
2. Wachungaji walipoona yaliyotokea walikimbia na kuanza kuhubiri.
Luka 8:34 "Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani."
➡️Bila kuona hawa Wachungaji wasingeenda kupeleka habari njema, wangeendelea na mambo yao.
Kuna Nguvu kubwa katika kuona.
◼️Nguvu ya kuona ikawafanya Wachungaji waende kwa spidi kuhubiri habari njema za YESU KRISTO Mwokozi.
3. Ibrahimu aligundua atapata shida watu wakiuona uzuri wa Mke wake wakati yeye na Mkewe wanakaribia Misri.
Mwanzo 12:11-12 " Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai."
4. Eliezari aliuona uzuri wa Rebeka ndio maana akaona Rebeka anamfaa Isaka kwa ajili ya Ndoa.
Mwanzo 24:16-17 " Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda.
Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe."
➡️Nguvu ya kuona ikasababisha Rebeka aolewe na tajiri Isaka ki urahisi sana.
5. Kuna watu hadi waone Miujiza ya YESU KRISTO ndipo watamfuata.
➡️Mfano hai ni huyu ambaye baada ya kukutana na Muujiza mkubwa wa Bwana YESU KRISTO hakuhubiriwa na Mtu kumfuata YESU Bali alimfuata mwenyewe.
Luka 18:43 "Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza MUNGU. Na watu wote walipoona hayo walimsifu MUNGU."
◼️Ni jukumu lako Mhubiri kukaa vizuri na YESU KRISTO ili adhihilishe Miujiza yake kupitia Wewe.
6. Nguvu ya kuona ilifanya kazi kwa Yakobo kumpenda Raheli na kufanya kazi bila kuchoka ili apate kulipa mahali.
Mwanzo 29:17-20 " Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso. Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo. Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu. Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda."
➡️Nguvu ya kuona ilifanya mambo ya ajabu sana kwa Yakobo.
➡️Nguvu ya kuona ilileta upendo wa ajabu wa Yakobo kwa Raheli.
◼️Nguvu ya kuona iliyochanganyikana na upendo iliifanya miaka 7 kuwa kama siku chache tu.
➡️Wewe ambaye unaona miaka imeenda au unaona miaka 2 ijayo ni mbali sana au unaona mwakani ni mbali sana kwa Yakobo baada ya kuona miaka saba ilikuwa kama siku chache tu na iliisha haraka sana akachukua Mke wa ndoto yake.
◼️Kuna Nguvu kubwa katika kuona.
➡️Zingatia tu Ukiona kwenye ulimwengu wa roho usiote kiburi ambacho huwapata baadhi ya watu baada ya kuona.
Mfano ni Hajiri alipoona tu Yuko mimba Tena mimba yenyewe ya tajiri Ibrahimu ambapo hata mahusiano yao hayakutokana na upendo ila yalitokana na mitazamo mibaya ya Sarah, Hajiri alipoona tu ana mimba akawa na dharau na kiburi kitu kilichofuata ni kufukuzwa.
Mwanzo 16:4 "Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake."
◼️Ndugu ukiona kwenye ulimwengu wa roho usipate kiburi Bali mtukuze MUNGU na Baki katika utakatifu uwapasao watakatifu walio katika KRISTO YESU.
◼️Ndugu, Mambo makuu ya MUNGU uliyoyaona maishani Mwako ni Akiba ya Baadae ili hata ikitokea umepitia wakati mgumu kabla ukumbuke na kumtukuza MUNGU hadi wakati ambao atakutendea.
Kumbu 4:9 "Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako;"
◼️Nini ufanye
1. Ishi Maisha Matakatifu ili kumruhusu ROHO MTAKATIFU kukuonyesha mambo ya Baadae.
Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."
2. Omba MUNGU akupe kuona kiroho yaliyo kusudi lake na akupe kuona yakupasayo kufanya.
Isaya 42:18 "Sikilizeni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona."
3. Fanyia kazi yale uliyoyaona kwenye ulimwengu wa roho.
Isaya 53:1 "Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani?"
4. Fanya Maombi sahihi baada ya kuona.
1 Wafalme 19:3 "Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko."
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments