NI KWELI UMETENDA DHAMBI LAKINI ISIWE TIKETI YA KUMWACHA YESU.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
Ukimaliza kujifunza Neno hili share kwa watu unaodhani watajifunza kitu.

◼️Ukisoma 1 Samweli 12:20-21 Biblia inasema "Samweli akawaambia, Msiogope; ni kweli mmeutenda uovu huu wote; lakini msigeuke na kuacha kumfuata BWANA, bali mtumikieni BWANA kwa mioyo yenu yote. Wala msigeuke upande, maana, kufuata vitu vya ubatili,"

➡️Maandiko haya yanayoonyesha Nabii Samweli akiwaambia Waisraeli waliofanya dhambi nyingi kwamba dhambi hizo zisiwe  sababu ya kumwacha MUNGU, mbele kidogo Samweli anaendelea kuwaambia  "Lakini kama mkiendelea kutenda mabaya, mtaangamia, ninyi na mfalme wenu pia.-
1 Samweli 12:25"

◾Tunajifunza Nini?

➡️Hata kama imetokea umekosea mbele za MUNGU rudi kwake kwa Toba na uache dhambi hiyo, maana hata ukichagua kuendelea na dhambi na kumkimbia YESU tambua kwamba mbele Yako Kuna kuangamia.

◼️Sifundishi ujumbe huu ili utende dhambi Bali nakuonya kama umeshatenda dhambi isiwe tiketi ya kumkimbia YESU KRISTO bali rudi kwake utubu kwa MUNGU na kuacha dhambi hiyo.

➡️Nasema haya kwa sababu Nina shuhuda nyingi za watu ambao walipokosea ndio walimwacha kabisa YESU na miaka michache baadae walikufa katika dhambi, ni mbaya sana.

➡️Nasema haya pia kwa sababu Kuna watu tangu alipokosea alilikimbia Kanisa, akawakimbia Wachungaji na akawachukia kwa sababu anadhani MUNGU hawezi kumsamehe.

◼️Kijana mmoja aliniambia kwamba Kwa dhambi alizotenda ana uhakika MUNGU hawezi kumsamehe hivyo amechagua kuwa yeye ni wa jehanamu hivyo nimwache tu aendelee kutenda dhambi zake, nikamfundisha kwa muda mrefu ndipo akaelewa na kuamua Kuokoka.

➡️Kuna watu baada ya kutenda dhambi mapepo humvamia na kumwambia ndani yake Kila mara kwamba hatasamehewa lakini huo ni uongo wa shetani maana MUNGU katika KRISTO YESU Ahadi yake ya daima inasema  "Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;-Isaya 1:18-19"

◼️Hii maana yake hata kama Mtu ametenda dhambi nyingi kiasi gani MUNGU anaweza akamsamehe.

➡️Dada mmoja aliwahi kuni-block Facebook kwa sababu Kila alipokuwa anafanya uzinzi akiingia tu Mtandaoni anakutana na somo langu linalokemea uzinzi akaogopa hadi akanichukia hivyo akaniblock ili asione Tena somo langu linalokemea dhambi yake, baada ya miaka 3 roho ikamuuma akaona aondoe block akaja hadi kunitembelea Kanisani ili nimuombee, Bwana YESU akamuondolea Mapepo na miaka miwili baadae akanipigia simu akisema hali yake ni nzuri na amejifungua Watoto mapacha wa kiume.

➡️Ndugu unayejifunza somo hili, ni kweli ulitenda dhambi nakuomba usimkimbie YESU, Rudi kwake kwa  Toba na kuacha dhambi hiyo  utasamehewa kabisa.

➡️Mwana mpotevu katika Biblia alikuwa amepotelea katika uasherati na dhambi lakini aliporudi kwa Baba yake alisamehewa, huo ni Mfano hai kwa watenda dhambi wote wakiamua kurudi kwa MUNGU katika KRISTO YESU yeye huwasamehe na haki zao za kwanza zilizopotea kwa sababu ya dhambi MUNGU huwarejeshea.

Luka 15:13,24 " Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.
................. kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia."

➡️Nimewahi kukutana na watu wengi walioamua kumwacha YESU baada ya wao kutenda dhambi mbaya.

◼️Kijana mmoja baada ya kutenda dhambi alivamiwa na mapepo hadi yakawa yanampatia mawazo ya kumtukana MUNGU, hivyo yeye baada ya kuwa na tabia hiyo ya kumtukana MUNGU akajihesabia  yeye ni wa jehanamu tu hivyo akaanza kutenda dhambi sana akidai hana Cha kupoteza kwani yeye ni wa jehanamu tu.
Aliponiambia nilimwambia kwamba MUNGU anaweza kumsamehe akiamua Kuokoka na Wala dhambi zake MUNGU hatazikumbuka akiokoka.

Waebrania 8:12 "Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena."

◼️Kijana mmoja aliniambia hivi "Mtumishi niache tu niendelee na Dhambi maana hata nikitubu siwezi kusamehewa maana nimefanya dhambi nyingi ikiwemo dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU "

Aliponiambia hivyo nikashtuka sana nikamwambia aniambie dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU aliyoifanya ni ipi.
Akanitajia dhambi hiyo nikamwambia dhambi hiyo sio dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU Bali ni dhambi ya Kawaida tu nikamwongoza Sala ya Toba akaanza upya na YESU.

Luka 15:10 "Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa MUNGU kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye."

➡️Katika utumishi wangu kwa KRISTO nilichogundua watu wengi baada ya kutenda dhambi shetani huwaingia na kuanza kuwadanganya kwamba waendelee tu na dhambi maana MUNGU hawezi  kuwapokea Wala kuwasamehe Tena, kumbe ni uongo ili watu hao waende jehanamu.

◼️◼️Ndugu Usikubali uongo wa shetani kamwe, Rudi kwa YESU KRISTO utasamehewa dhambi zako zote na Jina lako litaandikwa kwenye Kitabu Cha Uzima Mbinguni.

◼️Ndugu usimpe nafasi shetani kwenye Maisha Yako hata baada ya kutenda dhambi kwa bahati mbaya.

Waefeso 4:27 "wala msimpe Ibilisi nafasi."

◼️Ndio, dhambi ni mbaya sana ila ikitokea umeitenda tubu na Anza upya  na YESU KRISTO, usimkimbie maana ukimkimbia Kuna jehanamu mbele Yako.

◼️Omba MUNGU akupe Neema ya kuishinda dhambi.

➡️Ukichagua kumkimbia YESU kwa sababu umetenda dhambi ujue ndio unatafuta maangamizi zaidi.

➡️Daudi alipokosea alikiri kosa na kuhitaji msamaha wa MUNGU akaupata haraka sana.

2 Samweli 12:13 "Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa."

Daudi alitubu na kusamehewa.

Zaburi 51:4 "Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu."

◼️Ndugu, usimkimbie YESU KRISTO kama imetokea umetenda dhambi Bali tubu na kuiacha dhambi hiyo, ni hatari ukimkimbia YESU KRISTO.

◼️Dada mmoja ambaye hayuko katika Ndoa alizini akabeba mimba akaamua kukikimbia Kanisa na kuzidi kutenda dhambi, baadae wakamshawishi watu wabaya wakampeleka kwa mganga akafia huko kwa mganga wa kienyeji, ni hatari sana 

◼️Dada mmoja baada ya kutoa mimba 10 na Wanaume tofauti tofauti alidhani hawezi kusamehewa, siku Moja akakutana na somo langu akanitafuta baada ya kusoma somo langu mtandao akisema hawezi kusamehewa, nikamuongoza sala ya Toba, mapepo yakamtoka ,akaokoka na sasa anamtumikia MUNGU.

◼️◼️Ndugu Acha dhambi, ogopa dhambi, ikimbie dhambi lakini ikiwa umefanya dhambi ya namna yeyote ile rudi kwa YESU KRISTO haraka sana kabla hujachelewa, wafuate Watumishi wake Kisha amua kutoka moyoni kutokutenda dhambi hiyo Tena.
Kumbuka wale ambao Bwana YESU KRISTO aliwasemehe dhambi aliwaambia "Usitende dhambi Tena"

Yohana 5:14 "Baada ya hayo YESU akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi."

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments