![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
Leo tunaangalia Nini kinazaliwa na Uchungu.
➡️Maana 3 za Neno Uchungu.
◼️Neno "Uchungu" lina maana ya mateso ndani ya moyo wa Mtu yanayotokana na hali fulani iliyotokea.
Waebrania 12:15 "mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya MUNGU; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo."
◼️Neno "Uchungu" pia ni hali kubeba teso, chukizo au dukuduku baada ya kuumizwa.
Ayubu 15:20 "Mtu mwovu huwa na uchungu siku zake zote, Hata hesabu ya miaka aliyowekewa mwenye kuonea."
✓✓Huu ni uchungu unaokaa kwa watu waovu.
◼️Uchungu ni ile hali ya kuumia Moyo kwa sababu ya kitu alichotendewa Mtu au kilichomtokea Mtu.
➡️Watu wengi anapopata uchungu, huo Uchungu unamuelekeza kufanya mambo mabaya au kutenda dhambi.
Mfano hai ni Esau ambaye Uchungu wake ulizaa kutaka kuua, ni jambo baya sana.
Mwanzo 27:34 "Esau aliposikia maneno ya babaye, akalia kilio kikubwa cha uchungu sana, akamwambia babaye, Nibariki na mimi, mimi nami, Ee babangu."
Alipokosa baraka akamchukia Yakobo aliyebarikiwa.
Mwanzo 27:41 "Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo."
➡️Huyu Esau alikuwa anateswa na Uchungu wa kukosa Baraka.
➡️Watu wengine hupata Uchungu wa wivu kwa wengine, ni jambo baya sana.
Chanzo Cha uchungu huu na chuki hizi ni Mafanikio ya wengine.
Mfano ni huu
Nehemia 4:1 ''Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi."
◼️Mimi sijui Wewe Ndugu unapitia uchungu gani na Uchungu wa Nini ila Niko hapa kukuambia kwamba uige watu ambao walipopata Uchungu, huo Uchungu wao ulizaa Maombi na kuhitaji msaada wa Bwana YESU KRISTO na sio vinginevyo.
Ngoja nikupe mifano.
◼️Hannah alikuwa na Uchungu kweli lakini Uchungu wake ulizaa Maombi na kuweka nadhiri kwa MUNGU na akafanikiwa hitaji lake.
Uchungu ulimpeleka kwenye kuomba na kuweka nadhiri njema.
1 Samweli 1:10-11" Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe."
Hannah akafanikiwa.
1 Samweli 1:17-20 " Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na MUNGU wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba.
Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA."
◼️Mordekai Uchungu aliokuwa nao ulipelekea namna ya kutoka katika tatizo na Israel wote wakapona kupitia Yeye mwenye Uchungu.
Esta 4:1 "Basi Mordeikai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia pamoja na majivu, akatoka hata kufika katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu."
➡️Mordekai Uchungu wake ulimpa akili na maarifa ya kumweleza Esta aliyekuwa Ikulu na hiyo ikapelekea Waisraeli wote akiwemo na Esta na Mordekai Kufunga na kuomba kwa MUNGU hivyo msaada wa MUNGU ukatokea, walikuwa wafe wote ila hawakufa baada ya Maombi na kufanyia kazi maarifa ambayo ROHO MTAKATIFU aliweka ndani yao.
Esta 8:16-17 " Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi. Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, kwa kuwa hofu ya Wayahudi imewaangukia."
➡️Ndugu, Mimi sijui Wewe uko katika Uchungu gani, Uchungu ni mbaya na unaweza kuzaa madhara ya kiafya na Kiroho.
➡️Ndugu kama Wewe uko katika Uchungu unaokufanya utake kujiua, au kuharibu au kutenda dhambi hiyo ni mbaya sana Kwako, unaweza hata kukosa uzima wa milele kwa mambo mabaya uliyoyafanya baada ya Uchungu.
◼️Ukijiua unajipeleka jehanamu Moja kwa Moja kwa sababu umefanya Fanya ya kuua, hata kama ulikuwa Mtu wa Kanisani.
Waefeso 4:31 "Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;"
◼️Ndugu, hakuna tatizo la kudumu hivyo Uchungu usikutoe kwa YESU KRISTO Mwokozi.
Hata katika Uchungu nakuomba sana mtegemee MUNGU wa Mbinguni maana anaweza kukuponya na mabaya ambayo yangeletwa na Uchungu,zingatia sana hii.
Isaya 38:17 "Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa kunipenda umeniokoa na shimo la uharibifu; Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako."
◼️Ndugu nakuomba jitahidi sana kuushinda Uchungu maana Uchungu unaweza kuzaa mauti.
Ayubu 21:25 "Mwingine hufa katika uchungu wa roho, Asionje mema kamwe."
◼️Ndugu ushinde uchungu kwa kumkimbilia Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments