WATU 7 AMBAO MUNGU HUPENDEZWA NAO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

Leo tunaangalia watu 7 amabo MUNGU hupendezwa nao.


◼️Kama Kuna watu MUNGU wa Mbinguni hupendezwa nao ujue pia wapo watu ambao MUNGU hapendezwi nao, na watu hao ni watu wanaofanya mabaya.


Zaburi 5:4 "Maana huwi MUNGU apendezwaye na ubaya; Mtu mwovu hatakaa kwako;"


➡️Ujumbe wa Leo nazungumzia hasa watu wanaofanya mambo mema ambao MUNGU hupendezwa nao, kama Wewe unafanya dhambi au umemkataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wako dawa tu ni  kuacha mabaya na Mpokee Bwana YESU KRISTO kama Mwokozi wako ili uingie kwenye Kundi la watu ambao MUNGU hupendezwa nao.


Watu Saba ambao MUNGU hupendezwa nao.


1. MUNGU hupendezwa na Mtu mnyoofu wa Moyo.


1 Nyakati 29:17 "Nami najua, MUNGU wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao."


◼️MUNGU hupendezwa na unyoofu wa Moyo, na unyoofu wa Moyo huwa ndani ya Mtu hivyo MUNGU hupendezwa na Mtu kwa sababu ya unyoofu wa Moyo.


◾Unyoofu wa Moyo ni Nini?


◼️Unyoofu wa Moyo ni kitendo Cha Mtu kuacha misimamo mibaya Kisha kufuata mambo ya MUNGU bila kurudi katika misimamo mibaya ya awali.


◼️Unyoofu wa Moyo ni kitendo Cha Mtu kubadilika tabia na Matendo kutoka mabaya na Sasa akawa anatenda mema daima yampendezayo MUNGU.

MUNGU hupendezwa na watu wanyoofu wa Moyo


2. MUNGU hupendezwa na Watakatifu waliopo Duniani.


Zaburi 16:3 "Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao."


◼️Utakatifu huanza na kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako Kisha ukaendelea kufuata atakayo YESU kwa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.


◼️MUNGU hupendezwa na Mtu MTAKATIFU, Ndugu amua Kuokoka na kuishi maisha matakatifu ili umpendeze MUNGU wa Mbinguni.l, na MUNGU hukaa na Watakatifu.


Isaya 57:15 "Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu."


3. MUNGU hupendezwa na Mtumishi wake.


Isaya 42:1 "Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu."


◼️Mtumishi wa MUNGU ni Mtu yule anayemtumikia MUNGU katika KRISTO YESU.


Sio yule tu anayejiita "Mtumishi, Mchungaji, Nabii, Mwinjilisti, Mtumishi, Askofu n.k" Bali ni yule tu anayemtumikia, zingatia Mtumishi wa MUNGU ni yule anayemtumikia hata kama haitwi majina makubwa.


◼️Ukitaka umpendeze MUNGU Mtumikie katika KRISTO YESU.


◼️Ukitaka MUNGU apendezwe na Wewe Mtumikie Bwana YESU KRISTO.


4. MUNGU hupendezwa na Mtu anayezijua njia zake na kuzifuata.


Yeremia 9:24 "bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni BWANA, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema BWANA,"


◼️Kama wewe unazijua njia za MUNGU na unazifuata  MUNGU atapendezwa na Wewe.


◼️Amua kuzijua njia za MUNGU kwenye Kila eneo la Maisha Yako na zifuate ili umpendeze MUNGU.

Mfano njia ya kupokea kutoka kwa MUNGU ni Maombi, Kufunga n.k fanya daima hayo utampendeza MUNGU.


5. MUNGU hupendezwa na Mtu anayelishika Neno la YESU KRISTO.


Yohana 14:23 "YESU akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na BABA yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake."


◼️Jambo hili Muhimu sana watu wengi sana hawajui ndio maana MUNGU hajawahi kupendezwa nao, Ukitaka umpendeze MUNGU basi Shika Maneno ya YESU KRISTO na yafanyie kazi daima maana katika KRISTO YESU Pekee ndiko MUNGU amepitishia kusudi lake kwa Wanadamu wote.


Ukipuuzia maneno ya YESU KRISTO umempuuzia MUNGU hivyo hawezi kupendezwa na Wewe kamwe.


6. MUNGU hupendezwa na Mtu anayetoa Zaka na Sadaka kwa ukunjufu wa Moyo


2 Wakorintho 9:7 "Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu."


◼️Kama Kuna watu MUNGU hupendezwa nao ni pamoja na watu ambao humtolea MUNGU Fungu la kumi, Sadaka na dhabihu bila kushuritishwa Wala kulazimishwa, Bali wao hutoa kwa moyo wa upendo kwa sababu Wanampenda MUNGU.


◼️Ukitaka umpendeze MUNGU basi zingatia daima kuwa mwaminifu kwa MUNGU kutoa Zaka na Sadaka kwa moyo wa upendo na furaha ya Moyo.


7. MUNGU hupendezwa na Mtu anayempenda YESU KRISTO.


Yohana 16:27 "kwa maana BABA mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa BABA."


◼️Biblia Iko wazi sana kwamba MUNGU anatupenda kwa sababu tumempenda YESU KRISTO, Siri hii baadhi ya watu wa dini hawaijui lakini ni Siri ambayo anatakiwa kuijua Kila Mtu Duniani.


◼️Ndugu Ukitaka umpendeze MUNGU basi mpende Bwana YESU KRISTO Mwokozi.


➡️Lakini pia MUNGU Kwa wale anaowapenda huwarudi ili wasipotee wakaenda jehanamu.


Waebrania 12:6 "Maana yeye ambaye BWANA ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye."


➡️Pia MUNGU huwaponya watu anaopendezwa nao yaani watu ambao wameshika mambo 7 hapo juu.


2 Samweli 22:20" Akanitoa akanipeleka panapo nafasi; Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami."


◼️Ndugu, jitahidi sana usiwe miongoni wa watu ambao MUNGU hapendezwi nao kwa sababu hawajazingatia vipengele 7 hapo juu.


◼️Wewe zingatia vipengele 7 hapo juu ili MUNGU apendezwe nawe daima.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe

Comments