![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi. |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Yapo mapokeo Wanadamu wameyapokea lakini sio ya MUNGU hivyo wanapoyashika mapokeo hayo yanakuwa tu kama adhabu kwenye Maisha yao.
◼️Biblia ilitoa tahadhari mapema sana kwa Kanisa la KRISTO Duniani kwamba tusifanywe mateka kwa mapokeo ya Wanadamu au mapokeo ya story za zamani za kibinadamu.
Wakolosai 2:8 "Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya KRISTO."
◾Mapokeo ni Nini?
◼️Mapokeo ni desturi au utaratibu uliorithiwa kutoka kizazi hadi kizazi kingine.
◼️Yapo mapokeo ya Ki MUNGU kabisa na hayo ni mazuri sana na Yana maana sana.
1 Wakorintho 11:2 ''Basi nawasifu, kwa sababu mmenikumbuka katika mambo yote, nanyi mmeyashika yale mapokeo vile vile kama nilivyowatolea."
◼️Mapokeo ya Ki MUNGU ni mengi sana na Yana Nguvu ya MUNGU ndani yake, baadhi ya mapokeo hayo ni Kufunga Ndoa Kanisani, wanandoa kuvishana Pete ya Ndoa siku wanafunga Ndoa N.k
Mambo hayo hayamuondoi Mtu kwa YESU au katika utakatifu bali yampa Mtu kuweka Ahadi ya uaminifu kwa mwenzi wake mbele za MUNGU.
◼️Lakini Sasa sehemu kubwa zaidi ya mapokeo ni mapokeo wanayotembea nayo Wanadamu wengi ni mapokeo yasiyotokana na MUNGU wa Mbinguni na ROHO MTAKATIFU anayapinga ndani ya Wateule wake ambao wako naye.
◼️Biblia ilionya tangu zamani juu ya watu kufuata mapokeo yasiyo ya ki MUNGU.
Marko 7:13 "huku mkilitangua neno la MUNGU kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo."
➡️Ukisikia mapokeo yasiyotokana na MUNGU ujue mapokeo hayo yanatoka mojawapo ya sehemu hizi tatu;
◾Ni mapokeo yaliyoanzishwa na shetani au mawakala zake.
◾Ni mapokeo yaliyoanzishwa na Wanadamu kwa tamaa zao kwa wakati ule.
◾Ni mapokeo ya uongo ambayo yalibuniwa tu na watu waongo Kisha yakasambazwa na watu wanayafuata.
◼️Hata Imani zote nje na KRISTO YESU ni matokeo ya Mapokeo ya shetani na Wakala zake.
1 Yohana 2:18 "Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho."
◼️Na Watumishi wa MUNGU tangu zamani walionya kwamba akija Mtu Mwingine yeyote akileta analoliita Neno la MUNGU ambalo liko kinyume na Wokovu wa KRISTO YESU huyo alaaniwe maana anawaletea Wanadamu mapokeo ya kishetani ambayo wataishi wakifuata mapokeo hayo kama adhabu maana mapokeo hayo yatawapeleka jehanamu wote na sio Mbinguni maana kwa mapokeo hayo watamkataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wao.
Wagalatia 1:8-9 " Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi Injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi Injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe."
➡️Leo Kuna watu hadi hudhani watahukumiwa kwa kutokufuata mapokeo ya Wanadamu kitu ambacho sio kweli.
◼️Ndugu, utahukumiwa kwa kwenda kinyume na Neno la MUNGU katika KRISTO YESU na sio kuhukumiwa kwa kutokufuata mapokeo ya wazee wako.
Ndio maana nimesema Kuna mapokeo ni kama adhabu tu kwa wanaoyafuata.
◼️Mapokeo mengi ni ushetani ulio kinyume na Neno la MUNGU.
◼️Ndugu, ogopa sana ambacho hajaanzisha MUNGU, Wewe umekipokea tu kama mapokeo, ukifuata mapokeo hayo unamtukuza shetani aliyeyaanzisha.
➡️Leo Kuna hadi mapokeo ya "Kunywa kidogo ila usilewe" wengi walianzia hapo tu na Leo wanakunywa hadi wanajinyea na wengine baada ya kulewa na kupoteza fahamu walibakwa au Wanaume kuingiliwa kinyume na maumbile maana pombe huharibu akili ya Mtu.
◼️Aliyeambiwa anywe Mvinyo kidogo ilikuwa kwa ajili ya matibabu yake, alikunywa Mvinyo ule kama Dawa ya tumbo lake, Wewe Wala huumwi tumbo hadi upokee mapokeo hayo.
1 Timotheo 5:23-24 " Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara. Dhambi za watu wengine zi dhahiri, zatangulia kwenda hukumuni; wengine dhambi zao zawafuata."
➡️Leo Wahubiri kabisa wanafundisha kwamba watu wanywe kidogo ila wasilewe lakini hakuna aliyefundishwa kunywa kidogo Kisha baadae asiwe mlevi, hii ina maana Mtumishi amempoteza Mtu, maana pombe ni chanzo kikuu Cha mabaya mengi na dhambi.
Mithali 20:1 "Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; Na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima."
◼️Na Siri ambayo walevi wengi hawaijui ni hii "Mbinguni hakuna Mtu mlevi"
Biblia inasema walevi kama watenda dhambi wengine wataenda jehanamu.
1 Wakorintho 6:9-10 " Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi."
Sasa Wewe fundishwa kunywa pombe kidogo ila usilewe Baadae utakuwa mlevi ukifa katika ulevi utaenda jehanamu ndipo utamlaani mara milioni Mhubiri aliyekufundisha kwamba "Kunywa kidogo"
◼️Mapokeo kama hayo yamegeuka tu adhabu kwa wanaoyafuata.
➡️Kuna watu mapokeo yao ni kumkiri Mtume wao au Mtu aliyeishi zamani.
◼️Ndugu Neno la MUNGU linamtaka Kila Mtu amkiri MUNGU Baba wa Mbinguni na amkiri YESU KRISTO Mwokozi na sio wengine wowote.
Mithali 3:5-6 " Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako."
◼️Kumkiri YESU KRISTO kama Mwokozi wako ni faida Yako isiyo na kikomo, ni faida mpaka hadi baadae ukiondoka Duniani.
Mathayo 10:32-33 " Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni."
◼️Ndugu, Inawezekana Kuna mapokeo ya Wanadamu unayashika na hayo yanakutenga na uzima wa milele.
➡️Kuna watu hadi wamekatazwa Kuokoka kwa sababu tu watayaacha mapokeo ya wazee yasiyo na maana mbele za MUNGU.
➡️Kuna watu hadi wamekatazwa kusoma Biblia au kwenda Kanisani kwa sababu tu wakifanya hivyo Nuru ya KRISTO itakuja kwao hivyo watapata akili za kuyakimbia mapokeo ya shetani waliyoyashika tangu wakiwa Watoto wadogo.
◼️Ndio maana Bwana YESU KRISTO alikuwa mkali sana kwa watu waliolikataa Neno la MUNGU Kwa kufuata mapokeo ya Wanadamu.
Marko 7:8-9 " Ninyi mwaiacha amri ya MUNGU, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema! Mwaikataa amri ya MUNGU mpate kuyashika mapokeo yenu."
◼️Ndugu zangu Kuna watu walikuwa na mapokeo ya kunawa hadi viwiko, hicho sio kipaombele Cha Neno la MUNGU Bali ni mapokeo tu ya Wanadamu.
Mathayo 15:2-3 " Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. Akajibu, akawaambia, Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?"
◼️ Utakatifu hautengenezwi na kunawa mkono hadi kiwiko ndio maana kipaombele Cha MUNGU hakikuwa mambo ya kunawa mkono hadi kiwiko.
Marko 7:3-4 " Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba."
◼️ mapokeo mengine yanatokana tu na tamaa za ulafi wa baadhi ya watu.
➡️Niliwahi kwenda familia fulani kutembelea zamani, katika familia hiyo samaki anakatwa vipande viwili kati wakati wa kula hata kama mko watu 5 na ndani ya bakuli ya mboga Kuna vipande viwili vya samaki yaani kinchwa na mkia sehemu ya kichwa Cha samaki anakula Baba wa familia tu, na wengine wengine wote hata kama mko wengi mtagawana ule mkia wa samaki.
Watu wote wanajua kichwa Cha samaki ni Cha Baba wa familia na sio vinginevyo labda aje Babu ambaye amemzaa huyo Baba wa familia huyo ndio Pekee inabidi aachiwe hicho kichwa Cha samaki, na siku zote kichwa Cha samaki hukatwa kuanzisha kati kati ya samaki hivyo ni kichwa Cha samaki Jina tu ila ni zaidi ya nusu ya samaki mzima hata kama ni mkubwa kiasi gani.
Hapo Sasa Naamini unaanza kunielewa kwamba Mapokeo mengi hayatokani na MUNGU na yamekuwa tu adhabu kwa wanaoyafuata.
➡️Kwa ajili ya Mapokeo mabaya Leo Kuna makabila katika baadhi ya jamii za Kiafrika Mwanamke sio chochote kwa Mwanaume hata Kijana Mdogo ana Sauti kwa Wanawake wote hata kwa Mama yake Mzazi kwa Sababu ya mapokeo, inafika hatua wanadharau hadi wazazi wao wa kike.
Sasa ukifuata mapokeo ya kuwadharau Wanawake Wewe Mwanaume utamdharau hadi Mama Yako Mzazi, ukifanya kosa hilo ni hatari sana Kwako utapata madhara mabaya kulingana na Neno la MUNGU la Kweli ambalo linawahukumu Wanadamu wote na wa dini zote.
Walawi 20:9" Kwa maana kila mtu amlaaniye baba yake au mama yake hakika atauawa, amemlaani baba yake na mama yake; damu yake itakuwa juu yake."
➡️Unaweza usiishi miaka mingi Duniani Kwa kosa la kumdharau Mama Yako Mzazi kwa Sababu umefuata tu mapokeo ya kipepo.
◼️Ndugu, ukifuata mapokeo ya kutokuwaheshimu wazazi wako unalitamgua Neno la MUNGU na usubiri adhabu ya MUNGU
Mathayo 15:6 "basi asimheshimu baba yake au mama yake. Mkalitangua neno la MUNGU kwa ajili ya mapokeo yenu."
◼️Ndugu usishike mapokeo ya kishetani, Shika mapokeo ya Kiinjili.
2 Wathesalonike 2:15 "Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa waraka wetu.
Shika mapokeo ya kushuhudia mitaani"
➡️Shika Mapokeo ya Kuomba Kila siku mbele za MUNGU.
➡️Shika Mapokeo ya Kukaribisha watu Kanisani na sio kushika mapokeo ya Wanadamu.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments