![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU kwenye ujumbe huu wenye maana sana.
➡️Jifunze password ya majibu ya Maombi Yako kupitia somo hili ambalo Mimi Peter Mabula MUNGU wa Mbinguni amenipa Neema nikuletee Leo.
◾Saburi ni Nini?
◼️Saburi ni furaha ya Ahadi.
◼️Saburi ni furaha ya kupokea jambo Kabla halijatokea.
Waebrania 10:36-37 " Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya MUNGU mpate ile ahadi. Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia."
➡️ Ngoja nikupe ushuhuda huu kwa kweli.
Mama mmoja Mtoto wake alikuwa anaumwa sana ugonjwa wa Goita na alikuwa katika hali mbaya sana.
Kwa asiyejua Goita ni Nini, ni uvimbe mkubwa shingoni.
Katika Mtaa wao kukawa na mkutano mkubwa wa Injili.
Mama yule kama walivyo wengine akaenda kwenye Mkutano huo wa Injili kuanzia siku ya kwanza hadi ya Saba ambayo ilikuwa ya mwisho akiwa na Mtoto wake mgonjwa.
Mhubiri siku ya kwanza akaita watu Wenye mahitaji ili awaombee ili Bwana YESU awatendea, Mama yule naye akaenda akiwa na Mtoto wake akasema anahitaji aombewe Mtoto wake kwa ajili ya uponyaji.
Baada ya Maombi siku hiyo ya kwanza Mhubiri akaita watu Wenye ushuhuda Mama yule akaenda mbele akasema anamshukuru Bwana YESU KRISTO Kwa kumponya Mtoto wake.
Watu waliduwaa maana licha ya Maombi Mtoto alikuwa bado kwenye hali mbaya sana akiwa na hiyo Goita.
Kesho yake siku ya pili ya mkutano Mhubiri aliporuhusu watu wa kutoa ushuhuda yule Mama akaenda akashuhudia akisema "Anamshukuru Bwana YESU Kwa kumponya Mtoto wake" lakini Mtoto bado alikuwa na Goita ikionekana kwa macho, hivyo watu walikuwa wanamcheka na kumuona kama amechanganyikiwa.
Siku ya 3 ya mkutano Tena wakati Mhubiri alipoita watu wa kushuhudia yule Mama alikuwa wa kwanza Mhubiri akaamua kumuweka pembeni ili asishuhudie, hiyo siku ya tatu huyo Mama hakushuhudia.
Siku ya 4 Tena wakati Mhubiri anaita watu ambao wametendewa Miujiza na MUNGU yule Mama alikuwa wa kwanza na ushuhuda wake na ule ule, hakuna aliyemwelewa kuanzia Mhubiri hadi waliohudhuria mkutano huo wa Injili Inawezekana hata Wewe ungekuwepo usingemwelewa.
Hadi wakati ule Mtoto alikuwa bado mgonjwa, goita ilikuwa bado ipo na hali ilikuwa mbaya kwa Mtoto.
Siku ya 6 ya mkutano usiku wa siku wakati yule Mama na familia yake wanelala hiyo Goita ikaondoka ndani ya Mtoto wake, Mtoto akapona kabisa.
Mama anakuja kuamka asubuhi anakuta Mtoto wake hana uvimbe wa Goita na amepona kabisa.
◼️Mama huyu Maombi ya siku ya kwanza tu yalimfanya kuamini Mtoto wake amepona na hakutaka Kumsikiliza Mtu yeyote na baada tu ya Maombi Imani yake ilimpeleka jukwaani kushuhudia uponyaji wa Bwana YESU KRISTO Kwa Mtoto wake.
Yakobo 1:4 "Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno."
◼️Mama huyu Maombi ya siku ya kwanza tu aliamini MUNGU amefanya hivyo akabaki na saburi moyoni mwake.
Usiku wa Siku ya sita ya mkutano wa Injili ushindi wake dhahiri ulikuwa wazi kwake.
◼️Wakati Mwingine kama Mteule wa KRISTO Hakikisha una saburi.
2 Wathesalonike 3:5 "BWANA awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la MUNGU, na saburi ya KRISTO."
◼️Ndugu katika Maisha Yako ya Wokovu, Maisha ya Maombi, Maisha ya utoaji Zaka na Sadaka na dhabihu Hakikisha pia unakuwa na saburi.
Saburi imebeba uvumilivu unaleta ushindi wa lazima kwa mhusika.
1 Wathesalonike 1:3 "Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu YESU KRISTO, mbele za MUNGU Baba yetu."
◼️Kumbuka Waisraeli waliuzunguka mji wa Yeriko mara 6 bila kuona ushindi lakini siku ya saba ushindi wao ulionekana.
Ukuta wa Yeriko ulianguka na Waisraeli wakashinda.
Yoshua 6:20 "Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji."
◼️Ndugu Jifunze kuomba na kuamini Kisha msubiri MUNGU atende, Baki kwenye kuamini hadi Uone majibu Yako.
◼️Hata kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO kunahitaji Saburi, Ndugu Baki na saburi Yako daima wakati ukiishi Maisha Matakatifu.
Warumi 2:7 "wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele;"
➡️Ndugu umefunga mara chache mbona unakata tamaa?
➡️Umeomba mara chache mbona unanataka kuishia njiani?
➡️Umeokoka miaka 10 tu unaanza kuchoka? Ndugu wapo waliokaa kwenye Wokovu Miaka 90 na walipomaliza wakaenda kupumzika Mbinguni, wewe Miaka hii michache ndani ya Wokovu umeanza kuchoka?
Ndugu Hakikisha una saburi na Baki kwa YESU KRISTO daima.
➡️Umeomba mara kadhaa na kutoa Sadaka mara kadhaa tu lakini hadi umeanza kuwatukana kimya kimya Watumishi wa MUNGU waliokuombea.
Hebu Ndugu Kumbuka Mfano huu.
Bwana YESU aliuambia Mtini unyauke na wanafunzi wake waliona kabisa Mti ule haukunyauke wakati ule, lakini kesho yake walipofika eneo hilo wakashangaa ule Mti umenyauka.
Mathayo 21:19 "Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara."
◼️Wakati Mti unaambiwa unyauke haukunyauka wakati ule ila Neno lile lilianza kufanya kazi kufika kesho yake Mtu ule ulikuwa umeshanyauka.
Marko 11:20-22 " Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. YESU akajibu, akamwambia, Mwaminini MUNGU."
◼️Watu wengi sana ni waombaji ila Wana Imani haba na hawana saburi.
Ndugu Leo Nina uhakika ukizingatia Neno hili utakuwa na saburi na utaona majibu Yako mengi yanayotokana na Maombi Yako na utoaji wako kwa MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments