MAMBO 7 YATAKAYOIPANDISHA THAMANI YAKO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.

Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.

Naanza na mifano hai inayoonyesha thamani ya Mtu kuwa chini.


➡️Ukiona hawalii au hawahuzuniki baada ya Wewe kuondoka ujue pengo lako hawalioni.


➡️Ukiona haumii baada ya urafiki  kuvunjika ujue pengo lako halioni na thamani Yako kwake haipo.


➡️Unamuacha Mchumba Wala haumii au kuhuzunika, ujue pengo lako halioni na thamani Yako haionekani kwako.


➡️Unaaga Kanisani kwa sababu unahamia mkoa Mwingine kikazi watu Wala hawahuzuniki, sababu ni kwamba pengo lako hawalioni.


➡️Unaacha kuimba kwaya kwa sababu zako binafsi, siku unapotangaza kuacha kuimba watu Wala hawahuzuniki, sababu ni kwamba pengo lako hawalioni.


➡️Unahama kikazi lakini hapo kazini kwako siku unahama ndio wanafurahi na kushangilia na wengine wanajipongeza Kwa vyakula na vinywaji, kwanini iwe hivyo?

Sababu kuu ni kwamba watu hawalioni pengo lako.


◼️Hayo yote hutokea kwa sababu watu hawaioni thamani ya Mtu husika.


◼️Lakini Kuna watu thamani zao Ziko juu mno, yaani watu huwaambii kitu kuhusu Mtu huyo.


➡️Mfano ni huu ambapo Watu waliiona thamani ya Mtu mmoja aitwaye Daudi kwamba thamani yake ni kubwa kuliko watu elfu 10.


2 Samweli 18:3 "Lakini watu wakasema, Wewe usitoke nje; kwa maana tukikimbia, hawatatuona sisi kuwa kitu; au tukifa nusu yetu, hawatatuona kuwa kitu; lakini wewe u wa thamani kuliko watu elfu kumi katika sisi; kwa hivyo sasa ni afadhali ukae tayari kutusaidia toka mjini."


➡️Yaani heri wapate madhara watu elfu 10 kwa pamoja lakini sio kupata madhara Daudi aliye na thamani sana.


◼️Kuna watu thamani zao huonekana 


Maombolezo 4:2 "Wana wa Sayuni wenye thamani, Walinganao na dhahabu safi, Jinsi wanavyodhaniwa kuwa vyombo vya udongo, Kazi ya mikono ya mfinyanzi!"


➡️Vipi kwa Wewe ambaye thamani Yako katika familia yenu haionekani?


➡️Vipi kwa Wewe ambaye thamani Yako katika jamii haionekani?


➡️Vipi kwa Wewe katika ukoo wako wanakuona kama Mtu wa ziada tu kwa sababu thamani Yako hawaioni?


➡️Vipi kwa Wewe wanataka kukufukuza kazi kwa sababu thamani Yako hawaioni?


➡️Vipi kwa Mtu yule ambaye anataka kuachwa na Mchumba kwa Sababu thamani yake kwa Mchumba wake haionekani?

Leo Kuna nafasi katika Jina la YESU KRISTO kurudisha thamani za watu wengi.


◼️Leo nakupa Kanuni 7 za kuikuza thamani Yako.


1. Waheshimu watu wote na ishi vizuri  na Kwa amani na watu wote.


1 Petro 2:17 "WAHESHIMUNI WATU WOTE. Wapendeni ndugu. Mcheni MUNGU. Mpeni heshima mfalme."


◼️Heshima itakufanya uheshimiwe na ukiheshimiwa na watu Moja kwa Moja thamani Yako itaonekana daima.


2. Acha dhambi, maovu na makosa.


◼️Dhambi zote hupunguza heshima za anayezitenda.


➡️Mfano hai uzinzi hupunguza au kuondoa thamani ya Mtu.


Mithali 6:26 "Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani"


Wewe uliyeokoka ulinunuliwa kwa damu ya YESU KRISTO ya thamani sana, Hakikisha unatumia mwili wako katika Utakatifu na sio vinginevyo ili thamani Yako ibaki kuwa kubwa.


1 Wakorintho 6:20 "maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni MUNGU katika miili yenu."


◼️Usifanye mambo yanayoishusha thamani Yako, mambo hayo ni dhambi, maovu na makosa mbalimbali.


3. Tenda mema kwa watu wote.


Wagalatia 6:9 "Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho."


◼️Ishi Maisha ya kutenda mema Ukitaka thamani yako ionekane daima.


◼️Kutenda mema Kuna faida nyingi sana mojawapo ya faida ni kwamba mema Yako yatawaziba Vinywa wanaojaribu kuipunguza thamani Yako mbele za jamii, jamii haitawaelewa .


1 Petro 2:15 "Kwa sababu ndiyo mapenzi ya MUNGU, kwamba kwa kutenda mema mzibe vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu;"


➡️Je unamkumbuka Dorkasi yule ambaye thamani yake ilikuwa kubwa sana kiasi hata alipokufa Matendo yake kwenye Vinywa vya watu yalikuwa mazuri hadi akafufuliwa.


Matendo  9:36-40 " Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi."


➡️Dorkasi kwa sababu ya Matendo yake mema mengi alikuwa na thamani kubwa mno.

Leo Kuna watu akifa watu wanafurahi na kufanya sherehe, sababu ni kwamba thamani yake haipo mbele ya macho yao.


◼️Ndugu, kutenda mema kunaweza kuikuza sana thamani yake.

Usichoke kutenda mema katika KRISTO YESU Mwokozi na Kwa watu wote ili thamani Yako ionekane daima.


Waebrania 13:16 "Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo MUNGU."


➡️Mema makubwa zaidi ni pamoja na Uwe sababu ya watu kumcha MUNGU katika KRISTO YESU yaani Mtumikie Bwana YESU KRISTO Kwa uaminifu, walete watu kwa YESU KRISTO na thamani Yako itakuwa juu sana daima.


4. Tumia kipawa chako kwa hofu ya MUNGU na utakatifu ili kuifanya thamani Yako kuonekana.


Mithali 17:8 "Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa."


◼️Kama una kipawa kitumie katika KRISTO YESU na thamani Yako itakuwa kubwa daima.


◼️Kama ni Mhubiri hubiri sana na thamani Yako itaonekana daima.


◼️Kama ni mwimbaji imba sana na thamani Yako itaonekana daima.


◼️Kama mpiga kinanda pia kwa utukufu wa MUNGU na thamani Yako itaonekana daima.


◼️Kama ni Mwana Maombi omba sana na thamani Yako itaonekana daima.


◼️Kama ni Mwalimu fundisha sana.

Kama ni mtoaji endelea kumtolea MUNGU Kwa uaminifu na ukarimu na thamani Yako itaonekana daima.


◼️Kwa kazi yeyote katika KRISTO Fanya kwa juhudi na utakatifu na thamani Yako itaonekana daima.


Warumi 12:7-9 " ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema."


5. Kataa kiburi, kujiinua, kupenda sifa za kijinga na kudharau watu .


Mithali 29:23 "Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa."


◼️Kiburi Cha Mtu kitamshusha, na kikimshusha na thamani yake Moja kwa Moja itakuwa imeondoka.


◼️Ukitaka thamani Yako isionekame basi uwe na Kiburi, kujiinua na kupenda sifa za kijinga.


◼️Kataa mambo hayo matatu Ukitaka thamani yako ionekane daima.


6. Hakikisha una ROHO MTAKATIFU ndani Yako.


◼️ROHO MTAKATIFU ana kazi nyingi sana kwetu na kazi hizo zote hutufanya tuwe na thamani hivyo ukihitaji uwe na thamani daima basi Hakikisha una ROHO MTAKATIFU na unamtii.


◼️Mfano ROHO MTAKATIFU anaweza kukupa hekima kinywani Mwako  itakayokufanya usitamke kamwe mambo yatakayoishusha Thamani Yako.


Luka 21:15 "kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga."


◼️Kazi zote utakazozifanya katika ROHO MTAKATIFU zitakupa thamani kwa MUNGU na Kwa Wanadamu pia.


Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."


7. Jiendeleze kielimu na kiufahamu hasa kwa mambo ya MUNGU ili thamani Yako iendelee kuwa juu.


Mithali 3:13-15 " Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye."


◼️Nini ufanye katika Maombi 


1. Omba kwa MUNGU damu ya YESU KRISTO ya thamani ikusafishe na Wewe utakuwa na thamani


1 Petro 1:19 "bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO."


4. Omba Maombi ya kuiombea thamani Yako ili ionekane.


Marko 11:24 "Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu."


3. Kwa njia ya Maombi pambana na nguvu za giza zinazowinda thamani Yako.


Waefeso 6:11-12 " Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments