![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Ukisoma kitabu cha kutoka sura ya 2 kuanzia mstari wa 1-10 unaona namna MUNGU alivyo mficha Musa asiuawe na Wamisri.
Kumbe MUNGU anaweza kumficha Mteule wake katika KRISTO YESU ili asipate madhara.
➡️Kipindi hiki Mfalme wa Misri aliagiza Wakunga wawe wanawaua Watoto Waisraeli wa kiume wanaozaliwa na ndio kipindi hicho Musa naye alikuwa anazaliwa.
Kutoka 1:22 "Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai."
➡️Musa alifichwa wakati wa kuzaliwa, akafichwa ndani ya Safina ndogo akachukuliwa na binti farao akafichwa Ikulu hadi alipokuwa Mtu mzima.
Kutoka 2:2-10 " Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto. Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini."
◼️Musa alifichwa ili asiuawe maana Farao alikuwa anaua Watoto wa kiume.
◼️Kumbe MUNGU anaweza kumficha Mtu na mabaya yaliyokusudiwa kwa Mtu huyo yasimpate, hata kundi la Wateule wake MUNGU anaweza akawaficha ili wasipate madhara kutoka kwa adui zao.
Isaya 49:2-3 " Naye(MUNGU) anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake AMENISITIRI; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake AMENIFICHA; akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa."
◼️Malaika waliuficha mlango wa Lutu ili wabakaji wasiuone ili kuingia kufanya ubakaji.
Mwanzo 19:10-11" Lakini wale watu wakanyosha mikono yao, wakamwingiza Lutu kwao nyumbani, wakaufunga mlango. Kisha wakawapiga hao watu walioko mlangoni kwa upofu, wadogo kwa wakubwa, hata wakachoka kwa kuutafuta mlango."
➡️Ndugu Inawezekana uko Mtu unatafutwa kazini ili ufukuzwe kazi.
➡️Inawezekana uko Mtu Mtoto wako anatafutwa ili atekwe.
➡️ Inawezekana Yuko Mtu Mume/Mke wake anatafutwa atekwe kiroho.
➡️Inawezekana Mchungaji fulani anatafutwa atekwe ili kuua kazi ya MUNGU.
◼️Ndugu, MUNGU wa Mbinguni anaweza kukuficha na adui zako kiroho na kimwili wasikuone.
Mimi Peter Mabula nazijua Ziko fadhili nyingi za MUNGU, fadhili mojawapo ni MUNGU kukuficha dhidi ya Wanadamu wabaya ili wasitimize kwako makusudio yao mabaya dhidi Yako.
Zaburi 31:19 "Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako Ulizowawekea wakuchao; Ulizowatendea wakukimbiliao Mbele ya wanadamu!"
◼️Ukisoma Waefeso 6:12 unagundua uko na maadui wengi ambao uko nao katika vita wewe Mteule wa KRISTO.
Waefeso 6:12 ''Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."
◼️Omba MUNGU akufiche mbali na mipango ya siri ya mawakala hao wa shetani.
Ayubu 5:21-22 " Utafichwa na mapigo ya ulimi; Wala usiogope maangamizo yatakapokuja. Wewe utayacheka maangamizo na njaa; Wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi."
◾Kwa namna gani MUNGU anaweza kukuficha dhidi ya Watu wa wabaya au dhidi ya Nguvu za giza?
1. Mtu kukuficha na kumbe ni MUNGU amemtumia kukuficha.
Mfano hai ni huu wa Mama yake Musa.
Kutoka 2:2 "Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu."
2. MUNGU mwenyewe kukuficha kwa njia ya kwake.
Yeremia 36:26 "Mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, na Seraya, mwana wa Azrieli, na Shelemia, mwana wa Abdeeli, wamkamate Baruku, mwandishi, na Yeremia, nabii; lakini BWANA aliwaficha."
3. Ukikaa katika KRISTO kwa utakatifu na kulifanya kusudi la MUNGU uhai wako utafichwa pamoja na KRISTO katika MUNGU.
Wakolosai 3:3 "Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na KRISTO katika MUNGU."
4. MUNGU kuwapiga upofu adui zako ili wasikuone.
Luka 4:30 "lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake."
5. MUNGU kukupa neema na nafasi ya wewe kujificha ili usionekane na adui zako.
Yohana 8:59 "Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini YESU akajificha, akatoka hekaluni."
◼️Ndugu omba MUNGU akufiche dhidi ya adui zako kiroho na kimwili.
◼️Omba MUNGU akufiche dhidi ya mipango ya siri ya mawakala wa shetani dhidi Yako.
◾Nini ufanye katika maombi .
1. Omba toba na rehema ili uwe na haki mbele za MUNGU wa Mbinguni.
Zaburi 119:132-133 " Unigeukie, unirehemu mimi, Kama iwahusuvyo walipendao jina lako. Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki."
2. Omba MUNGU akufiche mbali na mipango ya siri dhidi yako.
Zaburi 64:2 "Utanificha mbali na shauri la siri la watenda mabaya, Mbali na ghasia ya watu wafanyao maovu;"
3. Omba MUNGU akuinulie watu kukusaidia ili usinaswe na adui.
➡️Mfano ni huu Binti Farao aliinuliwa na MUNGU Kwa ajili ya Musa ili amhifadhi.
Kutoka 2:9-10 " Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini."
4. Kwa Maombi pambana na adui anayekuwinda.
Yeremia 1:10 "angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda."
5. Omba MUNGU akulinde dhidi ya maadiu zako wa kiroho na kimwili.
Zaburi 64:1 "MUNGU, uisikie sauti yangu katika malalamiko yangu; Unilinde uhai wangu na hofu ya adui."
6. Omba katika jina la YESU KRISTO na utamwona MUNGU.
Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."
7. Mshukuru MUNGU amejibu Maombi Yako.
Zaburi 52:9 "Nitakushukuru milele kwa maana umetenda; Nitalingojea jina lako kwa kuwa ni jema; Mbele ya wacha MUNGU wako."
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments