![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
Warumi 8:37 "Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda."
◼️Ni Ahadi ya MUNGU kwetu tuliookoka kwamba tushinde na zaidi ya kushinda.
Ulishawahi kujiuliza unashindaje?
Kuna njia nyingi kiroho za kushinda Leo nakupitisha katika Ufunuo wangu huu.
◼️Ushindi wa mteule wa KRISTO unategemea anaona nini mbele za MUNGU anayemtegemea.
Mwanzo 21:19 '' MUNGU akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. ''
➡️Huyu anayezungumzwa katika andiko alikuwa anahitaji maji maana alikuwa jangwani yeye na mtoto wake, Macho yake yalikuwa hayaoni baraka yake ndio maana ikabidi ajitenge mbali na mtoto wake ili asione jinsi kijana wake atakavyokata roho baada ya kukosa maji kwa muda mrefu sana, ni neema ya MUNGU kwamba macho yake yakafumbuliwa na MUNGU hata akaona na kupata ushindi aliokuwa anauhitaji.
➡️Sijui kwa upande wako, inawezekana MUNGU kwa neno lake Biblia hukufumbua macho ili uone njia za kiroho za kuleta ushindi wako lakini huzingatii ndio maana hupati ushindi.
➡️Inawezekana unazingatia nusu tu au umejaa tu malalamiko na kujihesabia haki ndio maana hupokei.
◼️Yako mambo mengi unaweza ukaona mbele za MUNGU na kwa hayo ukizingatia unapata ushindi.
◼️Wakati mwingine unaweza ukaona mambo hata 7 mbele za MUNGU ili ukizingatia hayo ukutane na ushindi mkuu.
➡️Changamoto kubwa kwa baadhi ya watu ni kwamba macho yao ya rohoni hayaoni ndio maana hawazingatii kile alichowaonyesha MUNGU rohoni mwao.
Mathayo 6;22-23 '' Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo! ''
➡️Changamoto ya baadhi ya watu masikio yao hayasikiii na macho yao hayaoni ndio maana hawafuati maelelezo ya MUNGU juu ya kupata kwao ushindi.
◾Je wewe macho yako ya kiroho yanaona au hayaoni?
◾Je MUNGU alipokusemesha na kukufumbua macho ili uanze kuufuata ushindi wako ulizingatia?
◼️Wakati mwingine unaweza ukaona ushindi kupitia maombi, ukizingatia maombi hakika unapata ushindi.
◼️Wakati mwingine macho yako ya kiroho yanaweza yakaona ushindi wako kupitia Sadaka nzuri na maombi, ukizingatia unapata ushindi mkuu.
◼️Wakati mwingine macho yako ya rohoni yanaweza yakaona ushindi wako kupitia wewe kuwa na imani na kuvumilia na hakika utapata ushindi.
➡️Inawezekana wewe macho yako ya kiroho yanakuonyesha kwamba ili ushinde uhusike zaidi na damu ya YESU KRISTO ndipo ushindi wako utaupata, ukizingatia hakika unafanikiwa.
◼️Kumbuka ushindi wa mtu unategemea anaona nini.
➡️Kama huoni ni vigumu sana kupata ushindi.
◼️Ushindi wa mtu unategemea anaona nini, ana imani kiasi gani katika KRISTO YESU na anatarajia nini katika MUNGU.
◼️Jicho la rohoni linaloona ni la muhimu sana sana.
➡️Imani huwa ina macho na inaweza kuona, hivyo imani yako inaona nini juu ya hali yako?
➡️Je umeng'ang'ania kumsikiliza shetani anayekuambia kwamba MUNGU hatakusaidia.
➡️Je imani yako inaona uvumilivu kidogo maana utapokea.
Najua yuko Mtu anasoma ujumbe huu ila Yuko katika wakati mgumu sana na anaendelea na kuomba na kutoa, je macho yako ya rohoni yanaona vitu kama hivi ''Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. -Isaya 35:4''
➡️Inawezekana unaumwa sana au uko katika matatizo makubwa sana na unaendelea na maombi na utoaji na utakatifu, je macho yako ya kiroho yanaona hivi '' Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.-Ayubu 19:25 ''
➡️Je macho yako ya rohoni yanaona nini juu ya ushindi wako?
Siku moja miaka mingi iliyopita Mimi Peter Mabula nilikuwa naumwa sana na mawazo yangu yakatawaliwa na kifo maana nilijua sitapona, lakini ghafla utu wangu wa ndani ukanikumbusha juu ya ndoto fulani ambayo niliota zamani ikionyesha mambo ya miaka ya baadae kuhusu mimi, hivyo nikabadili mtazamo wa kuona kifo nikaanza kuona kupona na nilipoomba nilipona. Yaani ushindi wangu ulikuwa katika kuomba lakini ili niombe vyema nilitakiwa kukumbuka ahadi za MUNGU juu yangu.
➡️Inawezekana kuna siku MUNGU alikufunulia kwa maono au ndoto juu ya kwamba ipo siku utakuwa katika ndoa ukiwa na mwenzi wako pamoja na watoto hata zaidi ya wawili. Sasa hata kabla hujao au kuolewa unashangaa unaugua ugonjwa mbaya sana hadi mawazo yako yote yanatambua kwamba ndio unakufa, lakini kama ni MUNGU alikuambia juu ya mambo yako yajayo, basi unaweza kukumbuka na kuchangamka na kuomba kwa furaha.
◼️Kumbuka kazi mojawapo ya ROHO MTAKATIFU kwa wateule wa KRISTO ni kuwajulisha mambo yajayo, na yeye akisema ni kweli hakika.
Yohana 16:13 '' Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. ''
➡️Je macho yako ya rohoni yanaona nini juu ya ushindi wako?
➡️Je unazingatia?
➡️Je imani yako inakuelekeza katika jambo gani la Ki MUNGU ili upate ushindi, upone, ufunguliwe, uwe huru au uwashinde mawakala wa shetani?
◼️Ndugu, ushindi wako wakati mwingine unategemea unaona nini katika MUNGU aliyeziumba mbingu na dunia.
◼️Maombi yangu kwa waliokoka wenzangu ni haya ''macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake(MUNGU) jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; -Waefeso 1:18-19 ''
Naamini umejifunza jambo zuri na utafanyia kazi.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments