![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Leo tunajifunza kuhusu Macho ya MUNGU.
➡️Ukisoma 2 Nyakati 16:9 unaona kwamba Macho ya MUNGU huona Duniani mwote, Biblia inasema "Kwa maana macho ya BWANA hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita."
➡️Na hata Mtu anayefanya dhambi MUNGU humuona.
Waamuzi 13:1 "Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya BWANA, BWANA akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arobaini."
◾Mambo Saba Kuhusu macho ya MUNGU.
1. Macho ya MUNGU yapo kila mahali yakichunguza Mtu mbaya na Mtu mwema.
Mithali 15:3 "Macho ya BWANA yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema."
◼️Hivyo Mwanadamu yeyote huwezi kumkweta MUNGU Kwa namna yeyote ile, hivyo ni heri tu kumcha MUNGU katika KRISTO YESU Kwa utakatifu na uaminifu huku ukiishi Maisha safi yanayompendeza MUNGU wa Mbinguni daima.
2. Macho ya MUNGU huelekea wenye haki na kusikiliza Maombi yao.
1 Petro 3:12 "Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya."
◼️Kuna faida kubwa kuishi maisha ya haki, Maisha ya haki yatamfanya MUNGU akuangalie Kila Wakati na kusikiliza Maombi Yako.
◾Maisha ya haki ni Maisha gani?
➡️Maisha ya haki Kibiblia yamebeba maana tatu.
◼️Kwanza Maisha ya haki ni Maisha ya Wokovu katika KRISTO YESU Mwokozi.
Warumi 3:21-22 " Lakini sasa, haki ya MUNGU imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya MUNGU iliyo kwa njia ya imani katika YESU KRISTO kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;"
◼️Pili ni Maisha ya haki ni Maisha ya Mtu aliyetubu na kuacha dhambi akaambatana na KRISTO YESU.
1 Yohana 2:28-29 " Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake. Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye."
◼️Maisha ya haki pia ni Maisha Ukiwa ndani ya KRISTO usionee Mtu, usimchokoze Mtu na usitende mabaya kwa Mtu.
1 Yohana 3:10 "Katika hili watoto wa MUNGU ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na MUNGU, wala yeye asiyempenda ndugu yake."
3. Macho ya MUNGU yako kwa wamchao katika KRISTO YESU wanaongojea Fadhili zake.
Zaburi 33:18 "Tazama, jicho la BWANA li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake."
◼️Ingawa MUNGU anaweza kuwaangalia watu wote ila Kuna Kundi la watu huwazingatia ili awape msaada wake pale wanapouhitaji.
Watu hao ambao MUNGU huwazingatia ni wale wamchao katika KRISTO YESU huku wakingojea msaada wake.
◼️Ukitaka MUNGU akuzingatie na kukusaidia Kila Wakati basi Mche yeye katika KRISTO YESU Mwokozi.
4. Macho ya MUNGU huangalia utawala wenye dhambi ili kuwaondoa duniani.
Amosi 9:8 "Angalieni, macho ya Bwana MUNGU yanauangalia ufalme wenye dhambi, nami nitauangamiza utoke juu ya uso wa dunia; lakini sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo, asema BWANA."
◼️Falme zote Zenye dhambi MUNGU huziangalia na baada ya muda huziangamiza.
Wapo maelfu ya watawala wadhalimu MUNGU aliwaondoa katika madaraka maana ni tabia yake kuangalia utawala wenye dhambi ili kuuangamiza.
5. Macho ya MUNGU humhifadhi mwenye maarifa yake.
Mithali 22:12 "Macho ya BWANA humhifadhi mwenye maarifa; Bali huyapindua maneno ya mtu haini."
◼️Maarifa haya ni maarifa sahihi ya Neno la MUNGU la kuwasaidia watu wengi, Mtu wa namna hiyo anaweza kuhifadhiwa na MUNGU.
Tunayo mifano baadhi ni Kama Mtume Yohana ambaye aliishi miaka mingi sana ili maarifa ya MUNGU awape Vijana au kizazi Cha Vijana, Yohana hakuuishi tu muda mrefu Bali alikuwa na maarifa ya MUNGU Kwa faida ya Kanisa Zima la KRISTO Duniani.
Wako na Watumishi wengine wengi ambao waliishi miaka mingi wakilindwa na macho ya MUNGU ili maarifa ya ki MUNGU waliyoyabeba wanapatia Vijana.
◼️Kuna Mtu anaweza akalindwa sana na macho ya MUNGU Kwa sababu Mtu huyo ana maarifa ya ki MUNGU yatakayoisaidia jamii kubwa.
6. Macho ya MUNGU yapo mbele ya mwanadamu ili kumfanya MUNGU atafakari njia za wanadamu.
Mithali 5:21 "Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya BWANA, Na mienendo yake yote huitafakari."
◼️Wakati Mwingine MUNGU hutukagua mienendo yetu kwa kututazama.
◼️Wakati Mwingine MUNGU hutuangalia ili ajiridhishe kama kweli tunamcha Yeye.
7. Kuna eneo macho ya MUNGU yanaweza kuwako eneo hilo mwaka mzima .
Kumbu 11:12 "nayo ni nchi itunzwayo na BWANA, Mungu wako; macho ya BWANA Mungu wako, ya juu yake, tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wa mwaka."
➡️hii inaweza kuwa Kanisani kwenye madhabahu takatifu ya MUNGU ambayo watenda kazi wake hawaruhusu dhambi au uovu na wanamwabudu MUNGU katika ROHO MTAKATIFU na kweli.
◼️Pia eneo hili linaweza kuwa ni ardhi yoyote au eneo lolote atakalopenda MUNGU macho yake yawe huko mwaka mzima.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments