![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU juu ya mambo ya kutafakari Kila mara Wewe Mteule wa KRISTO ili yakufanye imara Kiroho.
Zaburi 104:34 "Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake; Mimi nitamfurahia BWANA."
◾Kutafakari ni Nini?
◼️Kutafakari ni kufikiri kwa umakini kuhusu jambo Fulani.
➡️Ni jambo zuri kutafakari ila Je unatafakari nini?
➡️Watu wengine hutafakari mambo yanayowaumiza tu kihisia na kiakili, hayo sio ya kutafakari.
➡️Kuna watu hutafakari maumivu au magumu tu na mambo mabaya yasiyo na Nafasi kwenye Maisha yao, hiyo haifai.
➡️Kuna watu hutafakari mambo ambayo ni dhambi, hiyo Ina hasara na sio faida kwao kiroho na kimwili.
◼️ Ndugu, Nakushauri uwe na tabia ya kudumu ya kutafakari hayo niliyokuandalia katika somo la Leo yanayotoka katika Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◾Mambo 7 Muhimu zaidi ya kuyatafakari Kila Wakati ni haya.
1. Mtafakari YESU KRISTO Mwokozi.
Waebrania 3:1 "Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, YESU,"
◼️Mtafakari Bwana YESU alivyokuokoa, alivyojitoa Msalabani kwa ajili yako.
Zaburi 63:6-8 " Ninapokukumbuka kitandani mwangu, Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku. Maana Wewe umekuwa msaada wangu, Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia. Nafsi yangu inakuandama sana; Mkono wako wa kuume unanitegemeza."
◼️Mtafakari Bwana YESU anakuandalia makao mazuri ya milele kama ukibaki katika Wokovu wake hadi mwisho.
◼️ Ndugu, litafakari Jina la YESU KRISTO ambalo kwa Jina hilo umeokolewa na unashinda.
Malaki 3:16 "Ndipo wale waliomcha BWANA waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha BWANA, na kulitafakari jina lake."
Ukiwa na muda mrefu Kila mara wa kumtafakari Mwokozi wetu YESU KRISTO hutakwama njiani, hutazimia Moyo Wala hutaacha Wokovu kamwe.
Waebrania 12:3 "Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu."
2. Tafakari mambo Mema ya Kweli na ya Haki.
Wafilipi 4:8 "Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo."
➡️Mambo mema ya kutafakari katika Maisha Yako yapo mengi sana, baadhi ni haya.
◼️Tafakari kufunga Ndoa Takatifu hata kama hauko katika Ndoa kwa Sasa au hata Mchumba hujapata.
◼️Tafakari kuzaa wazuri kama uko kwenye Ndoa na unamcha MUNGU wa Mbinguni.
◼️Tafakari namna utakavyopangilia kazi zako na upate muda wa Ibada na Maombi Kanisani.
3. Tafakari Maajabu na Miujiza ambayo MUNGU amewahi kukutendea.
1 Nyakati 16:9 "Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi; Zitafakarini ajabu zake zote."
➡️Hakuna Mtu hajawahi kutendewa Miujiza na MUNGU.
Zaburi 119:95 "Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako."
◼️Hata kukulinda na kuwakataza Wachawi kukudhuru ni Miujiza yake.
Zaburi 77:12-13 " Pia nitaitafakari kazi yako yote; Nitaziwaza habari za matendo yako. Ee MUNGU, njia yako i katika utakatifu; Ni nani aliye mungu mkuu kama MUNGU?
◼️Mfano hai mimi nimewahi kupata ajali zaidi ya Moja ila MUNGU wa Mbinguni akanilinda.
Niliwahi kuwa hospital na Daktari akasema damu yangu imechanganyikana na ubongo lakini pale pale Bwana YESU akanitokea na kuniponya, na mengine mengi sana hivyo ni lazima sana niwe na tabia ya kutafakari Maajabu ya MUNGU kwenye Maisha Yako.
◼️Ndugu uwe na tabia ya kudumu ya kutafakari Maajabu ya MUNGU kwenye Maisha Yako.
4. Tafakari Njia zako ili sehemu isiyo sawa utengeneze.
Hagai 1:7" BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu."
◼️Tafakari njia zako ili kama Kuna kitu umekosea kwa MUNGU utengeneze, kama Kuna sehemu umejisahau uweke mambo sawa mbele za MUNGU.
Zaburi 119:59 "Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako."
◼️Kitu Pekee ambacho Biblia inakataza kukitafakari ni mabaya uliyotenda zamani hata ukatamani kutenda Tena.
Usitafakari mabaya ya zamani hata ukatamani kuyatenda.
Isaya 43:18 "Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani."
5. Tafakari jambo la MUNGU au kazi ya MUNGU ili usishindane naye.
Mhubiri 7:13 "Tafakari vema kazi yake MUNGU; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?"
➡️Mfano Kuna Mtu ni wa Muhimu sana kwako ila amefariki na Wewe unaanza kusema "MUNGU kwanini umemuondoa"
Inawezekana Mtu huyo angeendelea kuishi angeikosa mbingu hivyo MUNGU akamuondoa kwa kumsaidia, au tu muda wake wa kuishi Duniani ulikuwa umeisha hivyo usishindane na MUNGU katika jambo lolote maana Wewe Mwanadamu hujui mengi.
➡️Kuna mambo mengi Yako kama yalivyo kwa sababu ni MUNGU ameyatengeneza hivyo au ametaka yawe hivyo, hivyo Tafakari kazi ya MUNGU ili usishindane naye.
Mimi Mfano niliwahi kuhama mkoa fulani ghafla tu kwa sababu ya mambo ya ajira wakati huo, wakati nahama nilikuwa najua Maisha yangu yote ningekaa mkoa huo, na Sasa nilikohamia sikupapenda hata kidogo, kwa miezi mingi nilikuwa katika huzuni kuu lakini huko ndiko milango ilifunguka hata nikaanza kujisemea "kumbe heri ningekuja huku miaka mingi iliyopita"
Kwa akili za kibinadamu za kawaida unaweza hata kulalamika kwa MUNGU kumbe ni MUNGU anakupeleka sehemu Bora zaidi kwako.
◼️Ndugu, uwe na tabia za kutafakari kazi za MUNGU au mambo ambayo utagundua ni MUNGU ametaka yawe hivyo.
➡️Mfano Mwingine siku Moja nilienda kwenye Ibada fulani ambako Mhubiri alikuwa raia wa nje ya Tanzania ambaye ni mlemavu wa miguu, lakini Mhubiri yule alikuwa na nguvu za MUNGU za ajabu sana, Miujiza mingi ilifanyika na hadi vilema walipona lakini aliyewaombea ni kilema, wao wakapona na kushangilia na kutoa Shuhuda ila aliyewaombea bado ni kilema.
Kwa akili za kawaida unaweza kusema "Mbona MUNGU hamponyi kwanza huyu Mtumishi mwenye upako mkubwa hivi"
Ndugu Tafakari kazi za MUNGU ili usishindane naye, vipi kama Mtumishi huyo asingekuwa kilema hata kwenye Ibada hiyo asingekuwepo au hata Kuokoka angekuwa hajaokoka bado, MUNGU hufanya baadhi ya mambo kwa sababu zake hivyo usishindane naye, Wewe mtukuze na mwelewe tu, na hiyo itakusaidia Ukiwa Mtu wa kutafakari kazi za MUNGU.
➡️Mfano Mwingine hujawahi kuona Mchungaji masikini ila unapompa Zaka akikuombea Wewe unafanikiwa sana kiuchumi?
Unaweza ukawaza mbona mwenyewe hajiombei ili awe tajiri, kwanini ana uwezo wa kuombea wengine wanakuwa matajiri ila yeye sio tajiri?
Ndugu Inawezekana naye Kuna wakati wake atafikia utajiri ila sio Sasa, Inawezekana MUNGU angempa utajiri sasa hata Uchungaji asingefanya, hivyo Ndugu mwelewe MUNGU Kwa kutafakari kazi zake hiyo itakusaidia usishindane naye.
6. Tafakari Neno la MUNGU.
Mithali 16:20 "Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye BWANA ana heri."
◼️Kuna faida kuu mno na nyingi kwenye kutafakari Neno la MUNGU.
◼️Ndugu, Tafakari Maandiko ya Biblia.
◼️Tafakari Mafundisho uliyofundishwa Kanisani au kwenye semina za Neno la MUNGU au kwenye majukwaa ya Watumishi wa KRISTO waaminifu mitandaoni.
◼️Tafakari Neno alilokwambia MUNGU kupitia Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU .
Zaburi 119:97 "Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa."
◼️Tafakari kile Roho mtakatifu amekuambia kwa sauti
Zaburi 119:15 "Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako."
7. Tafakari Neno la MUNGU katika kusoma, kuonya na kufundisha.
1 Timotheo 4:13-15 " Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha. Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee. Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote."
➡️Inawezekana Wewe ni Mtumishi wa MUNGU husika na mambo haya 3 katika kutafakari ili utimize kusudi la MUNGU kupitia Utumishi wako.
➡️ Inawezekana Wewe ni Mzazi tafakari Neno la MUNGU katika hayo 3 ili kuwasaidia Watoto wako na kizazi chako. `
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments