![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze kitu kupitia ujumbe huu mfupi.
◼️Kuna Matukio ya ajabu na Nyakati nyingi za ajabu zimewahi kutokea Duniani, hapa nimekuletea Chache katika ya nyingi.
➡️Nyakati hizi ziliambatana na matukio mbalimbali mbalimbali ya ajabu.
Mhubiri 3:1 "Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu."
◾ Matukio na Nyakati 5 za ajabu zilizowahi kutokea Duniani.
1. Neno la kweli la MUNGU kuwa adimu na kutokuwepo kwa Ufunuo wa MUNGU.
1 Samweli 3:1 "Basi, mtoto Samweli akamtumikia BWANA mbele ya Eli. Na neno la BWANA lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri."
✔️Huu ni wakati ambao MUNGU alikuwa amewanyamazia Wanadamu kwa muda mrefu.
◼️Wakati huu Neno la MUNGU lilikuwa adimu sana yaani lilikuwa haipatikani kwa sababu Wahubiri walikuwa hamna, labda Mhubiri alibaki Kuhani Elly na wenzake Wachache sana, Hata kuhani Elly naye alikuwa na udhaifu wa kutokukemea Dhambi hivyo Neno halisi la MUNGU lilikuwa Adimu sana.
1 Samweli 3:12-13 " Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho. Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia."
➡️Nyakati hizi ilikuwa Nyakati ngumu sana kwa sababu Neno la MUNGU lilikuwa adimu.
◼️Ukijua faida za Neno la MUNGU katika KRISTO YESU hutafurahi Neno hilo likiwa adimu kwa Wanadamu.
◾Hii ikufundishe Nini?
◼️Ikufundishe kwamba hata Wakati Wahubiri wa kweli wa Injili ya KRISTO katika Maeneo Yako hawapo au ni wachache Wewe hifadhi Neno la KRISTO hata kama Wengine hawafanyi hivyo, Mimi nimewahi kukaa eneo ambalo asilimia 98 sio Wakristo na hairuhusiwi hata kuwasha kwa Sauti kubwa redio inayopiga nyimbo za Injili, na wakati huo Mtumishi wa MUNGU Rose Muhando alikuwa ametoa albamu yake ya YESU Nibebe, nyimbo nyingi zinamtaja YESU hivyo watu wa jamii ile isiyo na YESU hawakutaka kusikia Jina YESU KRISTO, na siku Moja wakati nafua nguo nilifungulia nyimbo za Injili nzuri zinazomhubiri YESU mwenye nyumba nilipokuwa nimepanga akaniambia nihame kwenye Nyumba yake nikahama.
Na katika mazingira yake yale MUNGU alisema na Mimi kwamba nitajenga nyumba kiajabu sana na ikaja kuwa hivyo.
Lakini hata katika wakati huo ambao Neno la MUNGU lilikuwa adimu katika wilaya hiyo niliyokuwepo nilibaki na Neno la KRISTO kwa spidi ya ajabu zaidi.
✓✓Hata wewe lijue hili ya kwamba hata kama utakuwa sehemu ambayo Neno la kweli la MUNGU katika KRISTO YESU ni adimu Wewe uwe kama Samweli ambaye alibaki na MUNGU akiwa Mtoto Mdogo kipindi Neno la MUNGU ni Adimu kama andiko linavyosema hapo juu kwamba "Basi, mtoto Samweli akamtumikia BWANA mbele ya Eli."
2. Kila familia nchi nzima kufa Mtu Mmoja kwa usiku mmoja.
Kutoka 12:30 "Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu."
➡️Nyakati hii ngumu sana iliwakuta Taifa Zima la Misri, yaani Kila familia Mtu mmoja alikufa usiku Mmoja.
➡️Pata picha familia Moja waamka asubuhi Mtoto wa kwanza amefariki wanapokwenda kwa jirani kualika watu waje msibani wakifika hiyo nyumba wanakuta msiba au wakiwa wanaenda kwa jirani wanakutana njiani na majirani 5 na Kila mmoja anakuja kuita watu msibani kwake.
➡️Yaani ingekuwa kuna vikundi vya waombolezaji wa kuigiza kama ilivyo Leo siku hiyo hata waombolezaji hao wangeomboleza kiukweli ukweli Tena Kila mmoja na familia yake tu.
➡️Yaani kama familia ilikuwa ya Mtu mmoja tu naye kwa wazazi wake alizaliwa peke yake akiwa Mtoto wa kwanza na huku mama yake naye ni Mtoto wa kwanza na Baba yake naye ni Mtoto wa kwanza wangekufa wote asiwepo wa kuwazika kama majirani hawatajua.
➡️Nyakati hii ilikuwa ngumu kuliko kawaida kwa Taifa Zima.
Na ilitokea kwa sababu MUNGU alikuwa analipizia Waisraeli kisasi Cha utumwa wa miaka 400 na pia MUNGU alikuwa anajilipizia kisasi kwa miungu ya Misri.
Kutoka 12:12 "Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA."
◾Hii ikufundishe Nini?
◼️MUNGU anaweza kukulipizia kisasi kibaya kwa adui zako waliokutesa muda mrefu kama Wewe ni Mteule wa KRISTO unayeishi Maisha Matakatifu.
◼️Hii ikufundishe kwamba usimfanye mtumwa Mtu mwenye Agano na MUNGU maana ukiendelea kumfanya mtumwa na kumuonea ipo siku MUNGU atakuadhibu.
◼️Hii ikufundishe kwamba usimtese Mtu anayemwabudiwa MUNGU wa Mbinguni kama Wewe unaabudu miungu na uko kinyume na KRISTO YESU.
3. Jua na mwezi kusimama kwa Maombi ya Joshua
Yoshua 10:12-14 " Ndipo Yoshua akanena na BWANA katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni. Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao. Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizoandama baada yake, hata ikawa yeye BWANA kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa BWANA alipiga vita kwa ajili ya Israeli."
➡️Hii ilikuwa kubwa kuliko, yaani jua kusimama kusimama ili Israeli ashinde.
Dunia nzima Wanadamu wote Nina hakika walikuwa wanashangaa jua haliendi huku masaa yanaenda na ilipofika usiku wa mwezi kuonekana na mwezi nao ukasimama hivyo Wanadamu wakawa wanashangaa mwezi na jua vimesimama vikiendelea kuwaka kwa wakati mmoja, yalikuwa ni Maajabu ya Dunia, ingekuwa Leo kipindi Cha internet na mitandao ya kijamii sijui ingekuaje.
◾Ikufundishe Nini hii?
◼️Ikufundishe kwamba Maombi ya Mtu mmoja yanaweza kutenda kazi hata Dunia nzima.
Maombi ya Joshua ya kusimamisha jua yalifanya jua lisimame kwa watu wote Duniani.
◼️Wewe uliyeokoka Maombi Yako yanaweza kutenda kazi hata kwa Taifa Zima hivyo maadamu una YESU KRISTO usijidharau.
◼️Wewe unaweza usisimamishe jua ila unaweza ukasimamishi ajali au mauaji au mambo mabaya kwa Maombi Yako, hata kama Ndugu zako wako mbali Maombi Yako yanaweza kutenda kazi huko huko mbali waliko.
◼️Omba katika Jina la YESU KRISTO utamuona MUNGU wa Mbinguni.
4. Makaburi kufunuka waliozikwa humo kufufuka.
Mathayo 27:50-53 " Naye YESU akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi."
◼️Hili ndio Nyakati kubwa kuliko zote zilizowahi kutokea, hili ndilo tukio kubwa kupita yote yaani Watakatifu wote ambao walishafariki zamani wanahamia makazi mazuri ya Mbinguni yaani wanaenda Paradiso au pema peponi.
◼️Na tangu siku hiyo Mteule wa KRISTO pekee aliyeokoka anayeishi Maisha Matakatifu akifa huenda huko.
➡️Ila Mtu aliyemkataa YESU kama Mwokozi akifa huenda kuzimu akisubiri jehanamu.
Ndio maana tajiri mtenda dhambi alikuwa kuzimu na huku masikini Mcha MUNGU akiwa paradiso.
Luka 16:22-23 " Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake."
◼️Hii ikufundishe kwamba ukifa Ukiwa unaishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa KRISTO utaenda paradiso.
◼️Hii ikufundishe kwamba Bwana YESU Alipokuja kazi yake mojawapo ilikuwa ni kuwatengenezea makazi mazuri Watakatifu wa kabla hajaja na Watakatifu watakaoliishi Neno lake baada ya wao kumpokea yeye kama Mwokozi wao baadae.
➡️Kama huna YESU KRISTO ukifa huwezi kwenda pema peponi hata kama watu watakupamba kwamba uende pema peponi.
◼️Bila YESU KRISTO hakuna Uzima wa Milele hivyo mpokee Leo YESU KRISTO awe Mwokozi wako, usije ukasahau kamwe Wokovu wa KRISTO YESU.
5. ROHO MTAKATIFU kuwashukia Watu wakaanza kuongea lugha za mataifa mengine, lugha ambazo bila ROHO MTAKATIFU wasingeweza kuongea .
Matendo 2:5-12 " Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya MUNGU. Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?"
◼️Hili ni tukio kubwa sana na la ajabu sana yaani Mtu hujui lugha fulani lakini katika ROHO MTAKATIFU unaiongea wakati wa kunena kwa lugha.
Nyakati hii ilikuwa wakati wa ujio wa ROHO MTAKATIFU.
◼️Hii ikufundishe kwamba katika Maisha Yako ya Wokovu unamhitaji sana ROHO MTAKATIFU.
Kila Mkristo anatakiwa ahakikishe anampokea ROHO MTAKATIFU.
Naamini umejifunza jambo zuri na utafanyia kazi.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments