WATU WABAYA WAEPUKE

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki katika KRISTO YESU.

Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.


◼️Kuna watu ni wa kuwaepuka sana ili kutunza Imani Yako kwa YESU, kutunza  kiroho chako, kutunza  mwenendo wako katika Wokovu na ili kutunza utakatifu na kutunza Maisha Yako ya kiroho kwa ujumla.


Waefeso 5:10-11 " mkihakiki ni nini impendezayo BWANA. Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;"


◼️Biblia inakataza kushirikiana katika Matendo yasiyo na faida.


◼️Biblia inakataza kushirikiana katika Matendo ya mabaya ambayo yote hutoka kwa shetani.


➡️Kwanini ujiepushe na watu Hawa 5 ambao Leo nakuletea?


◼️Ni kwa sababu usipowaepuka watakufanya ufanane nao na kumkosa MUNGU.

Ni vizuri kujiepusha na njia za watu wabaya.


Zaburi 17:4 "Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri."


◾Watu 5 hatari wa kuwaepuka



1. Watu wapendao anasa wakijifanya wacha MUNGU kumbe sio.


2 Timotheo 3:4-5 " wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda MUNGU; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao."


◼️Biblia inasema watu hao ni wenye Mfano wa utauwa lakini sio watauwa.

Mtauwa ni Mcha MUNGU hivyo watu hao hujifanya wameokoka, hujifanya ni Watakatifu na kumbe hufanya Uovu.

Watu hai ni rahisi sana kuwaamini ukidhani ni Wateule wa KRISTO wenzako.

Mtu wa namna hiyo ukimgundua mwepuke sana, ukimwamini atakupoteza kwa kukufanya uione dhambi kuwa ni kitu Cha kawaida tu.


➡️Watu hawa anaweza kwenda kwa waganga wa kienyeji na Kanisani anaenda, anavaa hilizi au shanga na Kanisani anaenda, ni mchawi na Kanisani anaenda, watu hao ni hatari.


➡️ Biblia inawaita hawako baridi Wala hawako moto yaani hawajulikani kama wameokoka au hawajaokoka.


Ufunuo  3:15 "Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto."


➡️Usipojiepusha nao hao ni lazima watakufanya ufanye dhambi.


2. Watu ambao wanaanzisha mambo kinyume na MUNGU na     kuwashawishi watu kinyume na MUNGU.

                      

Matendo 5:37-38 " Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika.

 Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa,"


➡️Biblia inasema habari za Yuda Mgalilaya ambaye aliwavuta watu wengi Kisha akapotea, Biblia inasema Mtu wa aina yake ni wa kujiepusha nae.


➡️Watu wanaoanzisha mambo kinyume na MUNGU baadhi ni watu wa Kanisa, baadhi Wana siasa na wengine watu tu Maarufu n.k


➡️Leo Kuna watu wanaanzisha dini au Makanisa lakini hawana YESU KRISTO ndani yao hivyo wanawavuta watu na kuwapoteza.


◼️Muogope sana Mtumishi yeyote ambaye anaenda kinyume na Wokovu wa KRISTO YESU, Mtumishi wa hivyo kazi yake ni kupoteza watu wanaomfuata.


➡️Watu hawa wanaoanzisha mambo kinyume na MUNGU ni wengi sana na Wana maarifa mengi ya kuvuta watu, Ndugu jiepushe na watu hao.


◼️Kipimo kikuu Cha kuwajua watu hawa ni wanashawishi Dhambi, wanakataza watu Kuokoka, wanatengeneza taratibu za kishetani kupitia ushawishi wao kwa watu n.k


3. Watu wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume na injili ya KRISTO.


Warumi 16:17-18 " Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao. Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu KRISTO, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu."


➡️Watu hawa wengi hujifanya Watumishi wa MUNGU lakini hutumikia matumbo yao, wanapindisha Neno la MUNGU, ni wachonganishi, wakati Mwingine wanawaaminisha watu kuamini kwamba wao tu ndio wameitwa na MUNGU au ndio Watumishi sahihi.


 ➡️Kazi yao kuu ni kwenda kinyume na Mafundisho ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO, hao waepuke sana.


4. Watu wenye maneno yasiyo ya Injili, na watu wa mashindano ya elimu ya uongo 


1 Timotheo 6:20 "Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na maneno yasiyo ya dini, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo;"


➡️Watu hawa wengi sio Wakristo lakini Kwa akili zao za kishetani hujifanya wanaujua Ukristo kuliko hata Wakristo.


➡️Hawa hufundisha uongo kwa kutumia midahalo au majukwaa ya mitandao ya kijamii na Lengo lao kuu ni ili watu wamwache YESU wakose uzima wa Milele.


◼️Ndugu, hakuna Mtu Duniani anaweza kumfahamu Bwana YESU KRISTO hadi Mtu huyo awe na ROHO MTAKATIFU.


Mathayo 16:15-17 " Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe KRISTO, Mwana wa MUNGU aliye hai.

 YESU akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa MWILI NA DAMU HAVIKUKUFUNULIA HILI, BALI BABA YANGU ALIYE MBINGUNI.


➡️Hata Petro alimfahamu Bwana YESU KRISTO Kwa Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.

Na ROHO MTAKATIFU hakai na wapinga KRISTO hivyo haiwezekani kamwe mpinga KRISTO kuwafundisha watu Kwa usahihi kuhusu YESU KRISTO, watu Hawa ni wa kujiepusha nao sana.


5. Watu wa maswali ya upuuzi.

                    

Tito 3:9 "Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana."


➡️Wapo watu wamejaa maswali ya upuuzi kuhusu MUNGU, YESU KRISTO, ROHO MTAKATIFU, Wokovu na kuhusu mambo mema ya Imani yetu ya Wokovu wa KRISTO, watu hawa hawaulizi ili kujifunza bali wanauliza ili wakufanye utende dhambi au ukufuru na ili kukubadilisha akili upunguze tumaini lako kwa MUNGU katika KRISTO YESU, watu hao jiepusha nao sana maana Wana maswali ya kipuuzi.


◼️Yakatae maswali ya kipuuzi yote maana yatakutoa kwenye reli ya Wokovu au yatakuvuruga kiroho.


Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments