SABABU 7 KWANINI TUNAFUNDISHWA NENO LA MUNGU.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.

Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.


◾Kwanini tunafundishwa Neno la MUNGU?


◼️Ukisoma Zaburi 105:8 unaona Biblia ikisema MUNGU amewapa vizazi elfu Neno lake yaani ameamuru vizazi hivyo waende kwenye Neno lake, Biblia inasema"Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu."


➡️Kama Neno la MUNGU limeamriwa kwa vizazi elfu hiyo ina maana vizazi vyote vya Wanadamu hadi mwisho wa Duniani ili wampendeze MUNGU inawapasa kutembea kwenye Neno la MUNGU la Biblia Takatifu.


➡️Hiyo pia Ina maana kwamba MUNGU hutimiza Ahadi zake zilizo katika Neno lake, hutimiza Ahadi hizo kwa vizazi vyote.


➡️Hiyo pia Ina maana kwamba Neno la MUNGU ni la wakati wote, litafaa wakati wote na litatimiza kusudi la MUNGU Kwa Wanadamu wa vizazi vyote.


◼️Ukisoma pia  Mithali 16:20 unaona Biblia ikisema Kuna mema mengi katika Neno la MUNGU, Biblia inasema "Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye BWANA ana heri."


➡️Hivyo ni Muhimu mno kujifunza Neno la MUNGU na kukitafakari daima katika KRISTO YESU.


◼️Tahadhari kuu juu ya Neno la MUNGU ni kwamba haruhusiwi Mwanadamu yeyote katika vizazi vyote kulibadilisha Neno la MUNGU maana Neno la MUNGU halina makosa popote.


Mithali 30:5-6 " Kila neno la MUNGU limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio. Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo."


 ◾Kwanini tunafundishwa Neno la MUNGU?


1. Tunafundishwa Neno la MUNGU ili litugeuze tufuate kile MUNGU anataka kwetu .

 

Warumi 12:2 "Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu."


◼️Tunafanywa upya Nia zetu kwa Neno la MUNGU.


◼️Tunajua mapenzi ya MUNGU Kwa kujifunza Neno la MUNGU.


Tunapompokea YESU KRISTO kama Mwokozi kiroho tumezaliwa upya, tumezaliwa na MUNGU Kwa Neno lake hivyo inatupasa kuishi katika hilo Neno.


1 Petro 1:23 "Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la MUNGU lenye uzima, lidumulo hata milele."


◼️Tunajua namna Bora ya kumpendeza MUNGU Kwa kujifunza Neno lake katika KRISTO YESU.


◼️Tunaujua ukamilifu uwapasao Wateule wa KRISTO YESU Kwa kujifunza Neno la MUNGU.


2. Tunafundishwa Neno la MUNGU kwasababu MUNGU anataka neno lake likae kwa wingi ndani yetu.

                     

Wakolosai 3:16 "Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu."


◼️Neno la MUNGU likikaa kwa wingi ndani yetu litatufanya tuwe na tabia ya ki MUNGU.


◼️Tunafundishwa neno la MUNGU ili tujitambue na tutambue wajibu wetu kwa MUNGU na kwa ulimwengu. 


3. Tunafundishwa Neno la MUNGU ili tuwe thabiti katika Imani yetu kwa MUNGU katika KRISTO YESU.


Warumi 10:17 "Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO."


◼️Imani bila Neno la MUNGU la Biblia Takatifu ni Imani potifu.


◼️Imani bila Neno la KRISTO haiwezi kuwa Imani sahihi.


◼️Kama Wateule waa KRISTO inatupasa kujifunza sana Neno la MUNGU ili kuongeza Imani zetu kwa MUNGU.


4. Tunafundishwa neno la Mungu ili tujue njia njema itupasayo kuiendea.


Zaburi 119:133 "Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki."


➡️Kumbe hatua zetu za Maisha ni Muhimu tukatembea kwenye njia ambayo ni Neno la MUNGU.


◼️Neno la MUNGU ndio njia ya sisi kupita ili tufikie uzima wa milele.


◼️Neno la MUNGU ndio njia ya kutuongoza katika mema yote na katika kusudi la MUNGU.


5. Tunafundishwa neno la MUNGU ili tulitumie kwaajili ya kuleta ushindi katika Maisha yetu .


Ufunuo  12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."


◼️Tunashinda kwa Neno la MUNGU la Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU tunapoliishi au kulitumia katika Maombi.


6. Tunafundishwa neno la MUNGU ili tuache dhambi na tufuate utakatifu unaoelezwa na neno la MUNGU. 


1 Petro 1:14-17 " Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana IMEANDIKWA, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Na ikiwa mnamwita BABA, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni."


◼️Neno la MUNGU ndilo limeandika Nini ni dhambi na Nini hatutakiwi kufanya hivyo Neno la MUNGU ndilo hutufundisha tuache Dhambi.


7. Tunafundishwa Neno la MUNGU kwasababu neno ni Matakwa ya MUNGU na kitu alichokiamuru.


Isaya 55:10-11 " Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma."


◼️Neno la MUNGU li hai na hutenda kazi.

Naamini umejifunza jambo zuri na utafanyia kazi.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments