SIFA ZA NABII WA UONGO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe.


➡️Kumezuka wimbi kubwa la Watumishi wajiitao Manabii, kati yao wapo Manabii wa kweli Manabii wa MUNGU katika KRISTO YESU,  lakini pia wapo Manabii wa uongo, na katika Kundi la Manabii kwa ujumla wake walio wengi ni manabii wa uongo.


➡️Leo kuna Watu wamegeuza huduma ya Unabii kuwa cheo ndio maana ni rahisi tuu mtu unayemfahamu kama Mchungaji au Mwinjilisti au Mwalimu kujipa cheo kipya cha Nabii hivyo anataka watu mumwite nabii.

Biblia Iko wazi sana ikisema usiiamini Kila roho.


1 Yohana 4:1 "Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani."


◼️Usiiamini Kila roho maana yake usimwamini Kila Mtu umuonaye akizungumza, akifundisha, akihamasisha, akihubiri au akifanya kazi ambayo anaiita ni kazi ya MUNGU, mthibitishe kwanza kama kweli Mtu huyo ametumwa na Bwana YESU KRISTO.


Mathayo 24:24 "Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule."


➡️Watu kumuamini Kila Mtu imepelekea  Leo wapo Manabii wa uongo wengi.


◼️Kwanza hata Nabii wa kweli hapaswi kuwatangazia watu kwamba yeye ni Nabii bali kazi ya unabii wa kweli ndiyo itawafanya watu wamwite Nabii na kumtambua kama Nabii.


Kazi ndio ikutambulishe Wewe ni nani.

➡️Kuna uwezekano kabisa katika baadhi ya Maeneo Manabii wa shetani wakawa 450 huku Nabii wa MUNGU katika eneo hilo akiwa ni mmoja tu kama ilivyokuwa wakati wa Eliya.


1 Wafalme 18:22 "Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa BWANA; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini."


➡️Sasa unampimaje Nabii wa kweli na unampimaje Nabii wa uongo?


◼️Leo nakuletea njia za kumjua Nabii wa uongo kwa urahisi ili ujitenge nae mbali.


◾Sifa za Nabii wa uongo.


1.  Nabii ambaye akikuambia jambo ambalo ukilifanya linakutoa katika kweli ya KRISTO ujue huyo ni Nabii wa uongo.


➡️Mfano hai ni Elima mchawi ila Nabii.

Lengo lake ni kuzuia watu kuokoka.


Matendo  13:6-8 " Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, NABII WA UONGO, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la MUNGU. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani."


◼️Nabii yeyote anayekufanya uache kumtegemea YESU KRISTO kama Mwokozi wako huyo ni Nabii wa uongo na ni wakala wa shetani.


➡️Mfano Mwingine ni huu kwamba Nabii anakuambia jambo ambalo linakuwa kama alivyosema lakini Kisha anakuambia kwamba uitumikie miungu, huyo ni Nabii wa uongo usimfuate.


Kumbu 13:1-3 " Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda BWANA, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote."

    

 ◼️Kumbuka   Miujiza tu haimfanyi Nabii kuwa wa kweli maana hata manabii wa shetani hufanya miujiza.


2. Nabii akikuambia yaliyopotoka juu ya MUNGU wa mbinguni ujue huyo ni Nabii wa uongo.


Kumbu 13:5 "Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya BWANA, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru BWANA, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako."


◼️Manabii Hawa ni wale waliopotoka juu ya MUNGU.


➡️Anaweza akakukataza kuomba kwa Jina la YESU KRISTO, huyo ni Nabii wa uongo.


➡️Anaweza akakuzuia Kufunga na kuomba akidai ni yeye tu atakuombea.


➡️Anaweza akatunga uongo mbalimbali ili kupotosha mambo ya MUNGU.


3. Nabii anayemsingizia MUNGU kwamba amesema na yeye kumbe hajasema naye huyo  ni Nabii wa uongo.


Kumbu 18:20 "Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa."


➡️Nabii wa uongo siku yake nyingine ni kumsingizia MUNGU amesema naye na kumbe Wala MUNGU hajasema naye, anafanya hivyo ili watu wamwamini kwamba ni Mtumishi wa MUNGU na kumbe sio. 


◼️Ukimgundua Nabii wa uongo kama nae mbali sana.


4. Nabii anayekueleza majibu tofauti na ROHO MTAKATIFU aliyowahi  kukuambia ukathibitisha ujue huyo ni nabii wa uongo.


➡️Mfano hai ni Nabii Kijana ambaye aliambiwa na ROHO MTAKATIFU kwamba asile Chakula Wala maji.


1 Wafalme 13:17 "kwani nimeambiwa kwa neno la BWANA, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia."


➡️Lakini Nabii mzee ambae ni muongo muongo alimdanganya Kijana kwamba ametokewa na Malaika na kuambiwa amwambie ale Chakula kumbe ni uongo, hiyo itapelekea kifo Cha Nabii Kijana.


1 Wafalme 13:18 "Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la BWANA, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo."


➡️MUNGU huwa habadiliki, hawezi kusema hivi Kisha akasema tofauti.

Inawezekana na kwako liko jambo ROHO MTAKATIFU alikuambia na ukathibisha, Nabii wa uongo anaweza kukutoa katika kusudi hilo la MUNGU Kwa yeye kumsingizia MUNGU amesema naye.


5. Nabii anayefanya ibada za kishetani zilizo kinyume na YESU KRISTO na ROHO MTAKATIFU ni nabii wa uongo na ni nabii wa shetani.


➡️Mfano ni Manabii wa Baali ingawa walikuwa wanaitwa "Nabii" ila walikuwa Manabii wa  shetani.


1 Wafalme 18:25 "Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini."


◼️Hata Leo wapo watu wanaitwa "Nabii" ila katika ukweli wao wao ni Manabii wa shetani maana wanatumikia yeye.

Hawa ni mawakala wa shetani kabisa, jiepushe nao.


6. Nabii anayesema uongo kinyume na kweli ya MUNGU katika KRISTO ni nabii wa uongo.


Mathayo 7:15 "Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali."


◼️Kazi ya Nabii wa uongo ni kusema uongo na kudanganya watu ili wamwache YESU KRISTO na wajitenge mbali na MUNGU wa Mbinguni.

Hao jiepushe nao.


  ➡️Baadhi yao wametengeneza biblia zao wanajiita mungu wanamkataa YESU kama Mwokozi n.k

Hao kwenye Makanisa yao usijaribu kwenye katika Maisha Yako yote.


7. Nabii wa uongo anapotoa maandiko.


Matendo  20:30 "tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao."


◼️Nabii yeyote anayeenda kinyume na Neno la MUNGU katika KRISTO YESU ni Nabii wa uongo, jiepushe nae, hata kama Mwanzo alikuwa Mtumishi mzuri wa MUNGU.


   ◼️Ndugu umemjua nabii wa uongo 

    ◼️usimfuate aliko.


       ◼️usifuate uongo wake.


       ◼️mkatae.


Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments