![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Kuna watu ni adui wa MUNGU.
Nahumu 1:2" BWANA ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; BWANA hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; BWANA hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira."
➡️Kuna mambo Mwanadamu anaweza akayafanya hadi kufikia kiwango Cha kuwa adui wa MUNGU.
Waamuzi 5:31 "Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee BWANA."
➡️Ni mbaya sana Mwanadamu yeyote yule kufikia hatua ya kuwa adui wa MUNGU.
◼️Kama umefikia hatua ya kuwa adui wa MUNGU nakushauri sana amua kuokoka na Anza upya na Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
◾Watu walio Adui wa MUNGU ni hawa
1. Waabudu miungu ni adui wa MUNGU.
Kumbu 8:19 "Lakini itakuwa, kama ukimsahau BWANA, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka."
◼️Mtu yeyote akimwacha MUNGU katika KRISTO YESU na kuanza kuabudu miungu mingine yeyote ile anakuwa adui wa MUNGU wa Mbinguni.
➡️Huwa Kuna adhabu ya MUNGU Kwa miungu hivyo adhabu hiyo huwapata na hao watu wanaoabudu hiyo miungu.
◼️Mfano hai ni Wamisri ambao walikuwa wanaabudu miungu na MUNGU akasema anakuja kutoa adhabu kwa miungu ya Misri, adhabu hiyo iliwapata hadi watu wanaoabudu hiyo miungu.
Kutoka 12:12 "Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA."
◼️Hapa MUNGU katika kutoa Hukumu ya miungu aliua hadi Kila familia Mtu mmoja ambaye ni mzaliwa wa kwanza, hayo ni matokeo ya kuwa adui wa MUNGU Kwa kuabudu miungu.
➡️Narudia, ni kwamba MUNGU alikuwa anafanya hukumu juu ya miungu ya Misri lakini madhara yaliwapata na watu wa Misri.
◼️Ndugu,Mungu hataki hata utaje taje majina ya miungu.
Kutoka 23:13 "Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako."
➡️miungu ni shetani, mizimu, majini na kila nguvu za giza.
➡️miungu ni watu walijigeuza mungu au watu wasio na akili wanawaita mungu.
➡️miungu ni sanamu zote mawe au chochote ambacho watu hukiheshimu kiibada.
➡️miungu ni maroho ya kuzimu ambayo watu wanayaabudu
◼️ MUNGU wa kweli ni MUNGU Baba wa Mbinguni aliyejifunua kwa njia ya KRISTO YESU na anaabudiwa katika ROHO MTAKATIFU, kama uko nje na Wokovu wa KRISTO YESU wewe unaabudu miungu na sio MUNGU.
2. Adui wa MUNGU ni mtu yule anayekata kuokolewa na YESU KRISTO
Warumi 5:10 "Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na MUNGU kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake."
➡️Kumbe tulikuwa adui wa MUNGU kabla ya kupatanishwa naye kwa damu ya YESU KRISTO.
➡️Kumbe kama hujapatanishwa na MUNGU kwa Damu ya YESU KRISTO wewe bado ni adui wa MUNGU.
◼️Ili usiwe adui wa MUNGU ni kuamua tu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kuishi ndani yake tangu umempokea.
3. Wanaomwasi ROHO MTAKATIFU
Isaya 63:10 "Lakini wakaasi, wakamhuzunisha ROHO yake MTAKATIFU; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao."
➡️Zingatia walipomwasi ROHO MTAKATIFU wakawa adui wa MUNGU.
Hivyo kila anayemwasi ROHO MTAKATIFU ni adui wa MUNGU.
Kumwasi ROHO MTAKATIFU ni pamoja na kumkataa YESU KRISTO kama Mwokozi, kukataa kazi ya ROHO MTAKATIFU, kukataa ushauri wa ROHO MTAKATIFU n.k
◼️Ndugu, ni Muhimu sana kuzikubali kazi zote za ROHO MTAKATIFU na kuishi katika yeye ndani ya KRISTO YESU Mwokozi.
4. Mtu anyepigana na Mtumishi wa MUNGU wa kweli.
Zekaria 2:8 "Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake."
➡️Kwenye maandiko ipo mifano mingi ya watu walioamua kupigana na Mtumishi wa MUNGU na MUNGU akawa kinyume nao, Mfano ni akina Kora dhidi ya Musa n.k
➡️Kuna mambo ukiamua kumpinga Mtumishi wa kweli wa MUNGU katika KRISTO YESU Moja kwa Moja utakuwa unapingana na YESU KRISTO na unapingana na MUNGU Mwenyewe, hapo ni kama kuwa adui wa MUNGU.
Luka 10:16 "Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma."
➡️Kumbuka MUNGU atakuwa adui wa adui zako kama wewe ni Mteule wake.
Kutoka 23:22 "Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao."
➡️Hivyo wako watu ni adui wa MUNGU Kwa sababu watu hao wanapigana na Mtumishi wake mwaminifu katika KRISTO YESU Mwokozi.
5. Mtu anayemchukia MUNGU ni adui wa MUNGU.
➡️Wako watu humchukia MUNGU na kuwa adui zake.
Hesabu 10:35 "Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee BWANA, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao."
◼️Ndugu kama Kuna ambaye hutakiwi kuwa na uadui naye wa kwanza ni MUNGU aliyekuumba.
Akina Farao hawakumtambua MUNGU wakaishia kufa huku Musa na Wale wanaomtambua MUNGU wakiendelea Kuishi.
Zaburi 68:1 "MUNGU huondoka, adui zake wakatawanyika, Nao wamchukiao huukimbia uso wake."
◼️Kataa daima kuwa adui wa MUNGU katika Maisha Yako yote.
6. Mtu aliye rafiki wa Dunia ni adui wa MUNGU.
Yakobo 4:4 "Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU."
◼️Amua kutokuwa rafiki wa Dunia.
➡️rafiki wa Dunia ni Mtu anayependa dhambi kuvuta bangi au sigara au kunywa pombe au uzinzi au ufiraji au umakaya, Mtu anayependa maovu, makosa, kuabudu sanamu na kupenda mambo ya Duniani yaliyo machukizo kwa MUNGU.
7. Mtu asiyeitii sauti ya MUNGU ni adui wa MUNGU.
1 Samweli 28:16-18 " Samweli akasema, Kwa nini kuniuliza mimi, akiwa BWANA amekuacha, naye amekuwa adui yako? Yeye BWANA amekutendea kama alivyosema kwa kinywa changu; BWANA amekurarulia ufalme mkononi mwako, na kumpa jirani yako, yaani, Daudi. Kwa sababu wewe hukuitii sauti ya BWANA, wala hukumtimilizia hasira yake kali juu ya Amaleki; kwa sababu hii BWANA amekutendea hili leo."
➡️ Kumbuka Sauti ya MUNGU ni kile MUNGU anasema kwa njia ya ROHO MTAKATIFU .
➡️ Sauti ya MUNGU ni kile ambacho Bwana YESU KRISTO anasema.
➡️Sauti ya MUNGU ni Neno lake la Biblia Takatifu lenye maelekezo kwako.
➡️Ndugu, Je umekuwa adui wa MUNGU Kwa ajili ya Nini?
◼️Nakushauri tubu Leo na kuacha mabaya ili uwe Sasa Rafiki wa MUNGU na sio adui.
◼️Nakushauri amua Kuokoka ili Sasa uwe Rafiki wa MUNGU na sio adui, YESU KRISTO anakusubiri umpokee ili uokoke.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments