AINA 8 YA NENO LA MUNGU UNALOLIHITAJI SANA

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.

Karibu Tujifunze Neno la.


◼️Neno la MUNGU ni la Muhimu sana katika Maisha ya Kila Mkristo.


◼️Neno la MUNGU linaloachiliwa kwa ajili yako MUNGU huwa hataki  lirudi bure Bali anataka litimize makusudi yake yeye.


Isaya 55:11 "ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma."


◼️Neno la MUNGU ni la Muhimu sana katika Maisha yetu kama Wateule wa KRISTO na Lina kazi nyingi kwetu ikiwemo kutuponya na kututoa katika maangamizo kama tukiamua kulifuata na kulifanyia kazi.


 Zaburi 107:20 "Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao."


◼️Kwa ujumla Kila Mtu Duniani analihitaji sana Neno la MUNGU la Wokovu wa KRISTO YESU, ni heri anayelisikia na kulishika.


Luka 11:28 "Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la MUNGU na kulishika."


◼️Kama kweli Wewe ni wa MUNGU basi lishike Neno la Bwana YESU KRISTO analolitoa MUNGU Kila Leo Kwa ajili ya watu wote.


Yohana 14:23 "YESU akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na BABA yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake."


◼️Sasa Kuna aina nyingi za Neno la MUNGU unazozihitaji katika Maisha Yako, amua tu kufanyia kazi Kila Neno la MUNGU.


➡️Changamoto ya watu wengi huchagua tu Neno la MUNGU wanalolipenda au wanalolihitaji, hiyo imepelekea hadi baadhi ya Wahubiri kuacha kuhubiri aina nyingine za Mahubiri ili kuwafurahisha Wanadamu, Ndugu zangu haifai kuwa hivyo kamwe.


Rafiki yangu mmoja ambaye  ni mtaalamu wa kuwatengenezea Wahubiri video kwa njia ya ku-record na ku-edit siku Moja aliniambia hivi "Mtumishi Mabula kwa ninavyoangalia   Mahubiri Yako Kila siku mitandaoni unafanya kazi nzuri ila huwezi kuwa Maarufu kwa sababu umenyooka, Injili za kunyooka watu hawazitaki hivyo ili upenye kwa watu wengi inabidi uwe kama Mtumishi ........... Na Mtumishi .......... Ambao wao husema hata mambo ambayo yana ukakasi kiroho ili kuwavuta watu ndio maana Wana maelfu ya watu wanaowafuatilia, ulimwengu wa Sasa hauhutaji Injili za kunyooka kama za akina Moses Kulola" 


Rafiki yule baada ya maelezo yake akanionyesha video kadhaa mtandaoni za Watumishi zinazoenda viral sana, akasema watu wanataka Mahubiri kama hayo tu siku hizo.


Yaani ili watu wa Leo uwapate udanganye Mfano useme " nimemkamata Malaika Niko naye nyumbani kwangu, au kuoa Mke zaidi ya mmoja sio Dhambi, au tumia kafara kupata mali n.k


Eti watu ndio wanataka Injili hizo.

Hawataki useme "YESU KRISTO anaokoa ukimpokea Leo unaokoka",  watu hawataki Injili iliyonyooka wanataka Injili inayochanganywa uongo na ukweli kwa pamoja.


◼️Ndugu zangu, Neno la MUNGU li hai Tena Lina Nguvu na ROHO MTAKATIFU ndio hulitoa kwa ajili ya watu wote hivyo haijalishi ni Neno la MUNGU kutoka aina usiyoipendelea Wewe lifanyie kazi kwa sababu limeletwa na ROHO MTAKATIFU kwako.

Neno la MUNGU ni la Muhimu sana katika Maisha Yako yote, Kumbuka hata ulimwengu uliumbwa kwa Neno la MUNGU.


Waebrania 11:3 "Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la MUNGU, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri."


Hivyo unahitaji Kila aina ya Neno la MUNGU ili umpendeze MUNGU.


Nimekuletea aina 8 za Neno la MUNGU unalohitaji sana.

         

1. Neno la MUNGU la kukuonya.


Waebrania 3:13 "Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi."


➡️Kama hupendi kuonywa kwa Neno la MUNGU huwezi kumpendeza MUNGU.


◼️Ndugu likubali daima Neno la MUNGU lililobeba maonyo juu Yako.


2. Neno la kubadilisha msimamo wako ili ujue na ufuate kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU.


➡️Kama Wanadamu wakati Mwingine tuna mitazamo yetu kumbe ipo kinyume na MUNGU hivyo Neno la MUNGU lipo kwa ajili ya kutufanya tubadili mitazamo yetu ili kinyume na MUNGU wetu.


 ◼️ Mfano Ibrahimu alikuwa na mtazamo kwamba hatazaa na atakayerithi mali zake ni mfanyakazi wake aitwaye Eliazari ila Neno la MUNGU likamwambia atazaa hivyo akalifuata na kubadilika mtazamo wake na kweli akaja kumzaa Isaka.


Mwanzo 15:4 "Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi."


◼️Ndugu kubali kubadilishwa mtazamo na Neno la MUNGU, Kuna Neno huja ili Wewe ubadili mtazamo wako juu ya mambo mbalimbali, Neno la MUNGU ndio uhakika mkuu unaouhitaji katika Maisha Yako.


 ➡️Mfano Yehu Inawezekana hakujua  Watoto wake na wajukuu zake watakuwa wafalme wa Israeli lakini Neno la MUNGU likampa uhakika.


2 Wafalme 15:12 Hilo ndilo neno la Bwana alilomwambia Yehu, akisema, Wana wako watakaa kitini mwa Israeli hata kizazi cha nne. Ikawa vivyo hivyo.



3. Neno la toba.


 Mathayo 4:17 "Tokea wakati huo YESU alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia."


◼️Hili ni Neno la MUNGU Muhimu sana, hata Bwana YESU KRISTO akihubiri aina hii ya Neno la MUNGU.

Ndugu, MUNGU akikuletea Mahubiri yanayokutaka kutubu Hakikisha unatubu, MUNGU hataki watu wapotee ila anataka wote waifikie toba ya kweli.

 

2 Petro 3:9" BWANA hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba."


◼️Ndugu fanyia kazi sana Neno la MUNGU linalokutaka kutubu, usilikimbie kamwe Neno hilo.

          

4. Neno la ahadi inayokuhusu.

 

Warumi 9:9 "Kwa maana neno la ahadi ni hili, Panapo wakati huu nitakuja, na Sara atakuwa na mwana."


◼️Kuna Neno la MUNGU ni la Ahadi hivyo unapofundishwa hilo ongeza Imani Yako kwa YESU na endelea kumtegemea MUNGU maana Ahadi yake kwako itatimia.


◼️Yamkini MUNGU amewahi kusema na Wewe Kwa Neno, Ndugu lifanyie kazi Neno la Ahadi ya MUNGU kwako

            

5. Neno la kutakasa.


Yohana 17:17 "Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli."


◼️Ukikutana na Neno la MUNGU la kutakasa Hakikisha unajifakasa kwa damu ya YESU KRISTO maana Neno hilo sio Bure.


◼️Ukikutana na Neno la aina hii Hakikisha unaomba Maombi ya kujitakasa.


1 Timotheo 4:5" kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la MUNGU na kwa kuomba."


6. Neno la Faraja.


Mwanzo 15:1 "Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana."


◼️Ukikutana na Neno la faraja lisome na litafakari maana nalo kina kazi yake kwako.


2 Wakorintho 1:4 "atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na MUNGU."

  

7. Neno la kuponya.


Mathayo 8:16 "Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi,"


◼️Kuna aina nyingine ya Neno la MUNGU ni Neno la kuponya, lifanyie tu kazi katika KRISTO YESU na utapona ugonjwa wowote.


8. Neno la kubadilisha Mtu kutoka dhambi au msimamo mibaya ili sasa amfuate KRISTO na awe wa KRISTO.


Yakobo 1:18 "Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake."


◼️Neno hili Mtu akilifuata litamfanya azaliwe upya kwa Neno la MUNGU.

Mfano wake ni Mtu mzinzi au Mchawi au muongo anapilisikia Neno la MUNGU akalifuata kuanzia siku hiyo anaacha uzinzi au anaanza uchawi au anaacha uongo, huyo anayefanikiwa kuacha dhambi hizo baada ya kulisikia Neno la KRISTO anakuwa ni kama amezaliwa upya.

Ingawa kuzaliwa upya kuanza na Mtu kulisikia Neno la MUNGU akampokea YESU KRISTO na kuacha dhambi zote.


1 Petro 1:23 "Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la MUNGU lenye uzima, lidumulo hata milele."


➡️Ndugu. Neno la aina hii kamwe usije ukaliacha liende tu Bali lifanyie kazi binafsi.


◼️Neno la aina hii  kuhuisha yaani kumfanya Mtu aliyekufa kiroho kwa sababu ya dhambi awe mzima sio aliyekufa Tena.


       Zaburi 119:107 ''Nimeteswa mno; Ee BWANA, unihuishe sawasawa na neno lako."


    ➡️  Kuhuishwa ni kufanywa upya  kiroho.


  ➡️ Kuhuishwa ni kuongezewa nguvu kutoka kukata tamaa ili Sasa usonge mbele.

Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments