![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
Leo tunajifunza jinsi ya kuishinda hofu
◾Hofu ninini?
◼️Hofu ni kuogopa kukabiliana na jambo.
➡️Kuna mambo huleta hofu, na Kuna watu Wana Moyo wa hofu ila katika KRISTO YESU Kuna njia za kuishinda hofu yeyote inayotokea.
Isaya 35:4 "Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, MUNGU wenu atakuja na kisasi, na malipo ya MUNGU; atakuja na kuwaokoa ninyi."
◼️Maana nyingine ya Hofu ni hali ya kutokuwa na ujasiri.
Kumbu 20:3 "awaambie, Sikizeni, enyi Israeli, hivi leo mwasongea mapiganoni juu ya adui zenu mioyo yenu na isizime; msiche, wala msiteteme, wala msiingiwe na hofu kwa ajili ya wao;"
➡️Lakini Ukiwa na MUNGU wa Mbinguni utashinda hofu zote, na MUNGU hataki tuwe watu wenye hofu.
◼️Maana ya tatu ya neno "Hofu" ni hali ya uoga inayopelekea mtu kuonekana na sababu Fulani.
➡️Najua Kuna vitu huleta hofu.
Mfano ni hili
Zaburi 18:4 "Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu."
◼️Ila Leo katika KRISTO YESU Mwokozi tunajifunza namna ya kuishinda hofu inayotokea.
◾Je unataka kuishinda hofu?
◼️Mambo ya kufanya ili kuishinda hofu.
1. Kumwamini MUNGU atakuwa ngao kwako katika hatari zote.
➡️Kumbuka MUNGU alisema atakuwa ngao kwa Ibrahimu ndio maana Ibrahimu hakutawaliwa na hofu.
Mwanzo 15:1 "Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana."
◼️Hata Leo MUNGU ni ngao ya thamani kwa Wateule wake katika KRISTO YESU, hivyo hatutakiwi kutawaliwa na hofu.
◼️ Ndugu, Mwamini MUNGU katika KRISTO YESU kwamba atakuwa ngao Yako ya thamani hivyo hofu Wala haitakutawala Wala haitachukua nafasi ndani Yako.
2. Ishi Maisha matakatifu katika KRISTO YESU hofu itakukimbia.
Isaya 54:14 "Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia."
➡️Dhambi ni chanzo kimojawapo Cha Mtu kutawaliwa na hofu.
Biblia Iko wazi sana kwamba watenda dhambi hukimbia kwa hofu hata kama hakuna anayewakimbiza ila wenye haki yaani wanaoishi Maisha Matakatifu ni majasiri kama simba.
Mithali 28:1 "Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba."
◼️Majasiri kama simba hawawezi kutawaliwa na hofu, hivyo amua kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO na hofu itakukimbia Wewe.
3. Omba MUNGU akuponye na mambo yanayokupa hofu.
Zaburi 34:4 "Nalimtafuta BWANA akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote."
◼️Katika Maombi Yako katika Jina la YESU KRISTO yataje hayo yanayokupa hofu na omba MUNGU wa Mbinguni akuponye dhidi ya hayo yanayokupa hofu na hiyo hofu itaondoka ndani Yako.
4. Mwamini ROHO MTAKATIFU anaposema na wewe ndani yako.
Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."
◼️Moja ya kitu Cha Muhimu sana sana ili kushinda hofu ni kumwamini ROHO MTAKATIFU anaposema ndani Yako, akisema na Wewe ROHO MTAKATIFU ukiamini hofu itakimbia hata kama unaona hatari.
Ngoja nikupe ushuhuda huu ambao Mimi mwenyewe Peter Mabula ulinikuta.
Siku Moja nilikuwa katika vita Kali sana ya kiroho kiasi kwamba nilikuwa naona mauti.
Lakini katikakati ya hatari hiyo ndani yangu nikakumbushwa ndoto ambayo niliwahi kuiota zamani ikinionyesha Mimi nitakavyokuwa Baadae katika huduma na Maisha, nilipokumbuka tu nikajikuta najisemea kwamba "Kama MUNGU alisema na Mimi juu ya baadae yangu hakika hiyo Baadae nitafika, sitaishia hapa, sitakufa Bali nitaishi na nitafikia katika yake mema ambayo ROHO MTAKATIFU aliwahi kusema na Mimi" nilipowaza tu hivyo hofu iliyeyuka na nikaanza kuona ushindi na vita vikaisha.
Kwanini ilikuwa hivyo?
Kwa sababu MUNGU si Mwanadamu hata aseme uongo, yeye alisema nami juu ya kesho yangu hivyo mawakala wa shetani hawawezi kunizuia kufika katika kusudi la MUNGU wangu.
◼️Hata Inawezekana uko katika hofu kuu kwa sababu ya mazingira Yako ya Sasa ila yazingatie sana yake ambayo ROHO MTAKATIFU anakufunulia au kukusemesha kwa ndoto au Maono, mengine inaonyeshwa ili uwe na amani na hofu Yako iondoke maana MUNGU atatenda alichokufunulia.
Mfano mmoja Kuna Dada mmoja alikuwa kwenye mazingira magumu sana kwa sababu ya kuchelewa kuolewa, Ndugu zake walimwijia juu sana, shinikizo lilikuwa kubwa sana na yeye mwenyewe akakata tamaa kabisa ya kuolewa.
Lakini katikakati ya mazingira hayo hayo magumu ndoto zake Kila mara aliona ana familia na Mume na Watoto 2, Kila akiomba anaona hivyo, yeye alitamani MUNGU amfunulie akichumbiwa au akipata Mchumba au akifunga Ndoa, hapo kidogo angepata amani na tumaini lakini kumbe alikuwa anafunuliwa mambo ya mbele zaidi yaani ataolewa na atazaa Watoto na ndivyo ilivyokuwa baadae, Ndoa ilikuja ghafla na alichofunuliwa kilikuja kuonekana Baadae.
Hii maana yake Kuna mambo ya baadae unaweza ukafunuliwa ili ikitokea umepitia mazingira magumu kabla ya muda huo ukumbuke na hofu iondoke kwako maana Bwana YESU atatimiza alichokuambia.
◼️Kumbuka ROHO MTAKATIFU hutufunulia mafumbo yote ili tuwe na amani maana hayo mema yetu yatatimia.
1 Wakorintho 2:10 "Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."
◼️ Ndugu ukikumbuka alichokuambia MUNGU hata hofu ikija hutaogopa maana tunamwamini MUNGU aliyesema nawe maana atatimiza.
5. Mjue MUNGU ili uwe na amani maana hofu haiendi au haikai sehemu yenye amani ya MUNGU.
Ayubu 22:21 "Mjue sana MUNGU, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia."
◼️Ukijifunza sana kuhusu MUNGU katika KRISTO YESU utakuwa na amani, na hofu huwa haikai kwenye amani hivyo kujifunza kuhusu MUNGU kutaondoa hofu kwako.
◼️ Kumbuka Katika KRISTO YESU yote yanawezekana.
Zingatia mambo haya 5 na hofu haita kusumbua.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments