![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Kuna madhara yanayoweza kuletwa katika familia na Kiongozi wa familia husika.
◼️Kiongozi wa familia anaweza kuwa ni Baba wa familia au Mama wa familia.
➡️Mfano hai Leo Kuna watu wa MUNGU wengi Maombi yao Kila mara ni kuvunja laana za familia, kuharibu mizimu ya ukoo n.k
Hivyo wanavyoviharibu kwa Maombi ni vitu halisi kabisa ila vililetwa na ama wazazi wao au Babu zao hivyo Kiongozi wa familia wa Sasa jitahidi sana usiwe sababu ya wajukuu zako baadae wafunge na kuomba siku nyingi wakiharibu kazi za giza ambazo ni Wewe ulizileta katika wakati wako.
➡️Hivyo tukiwa kama Viongozi wa familia wa Sasa ni vizuri sana kumcha MUNGU katika KRISTO YESU ili kuepuka kuleta madhara kwa familia zetu.
Kumbu 7:26 "na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa."
◼️Neno "nyumba" Kibiblia Lina maana zaidi ya Moja na maana mojawapo ni familia uliyoianzisha wewe yaani Wewe na Mke wako na Watoto wenu.
◼️Kumbe Kuna machukizo Kiongozi wa familia anaweza akayaleta katika familia yake ndio maana Biblia hapo juu inasema " Usiweke machukizo ndani ya nyumba Yako"
➡️Kuna mtu alijifunza uganga mpaka sasa Watoto wake na wajukuu na vitukuu ni waganga wa kienyeji ambao wanatumia uchawi na majini na wamefanyika mawakala wa shetani familia nzima.
➡️Kuna mtu alijifunza uchawi kwao na kuwafundisha Watoto wake na kuleta madhara mabaya katika familia yake.
➡️Kuna mtu kwa tamaa zake alioa wake 2 watoto wakarithi na wajukuu na kuwa chukizo kwa MUNGU.
➡️Kumbe kuna mtu anaweza kuweka machukizo kwenye nyumba yake yaani familia yake.
◼️Lakini pia zipo familia zinazoweza kubarikiwa kutokana na Kiongozi wa familia husika.
Mfano ni huu
Ruthu 4:12 "Nyumba yako na ifanane na nyumba yake Peresi, ambaye kwamba Tamari alimzalia Yuda, kwa wazao atakaokupa BWANA katika mwanamke huyu."
◼️Nyumba inaweza kubarikiwa kwa sababu ya maamuzi ya mkuu wa familia hiyo.
Mfano ni huu
1 Nyakati 13:14 "Sanduku la MUNGU likakaa na jamaa ya Obed-edomu, nyumbani mwake, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akaibariki nyumba ya Obed-edomu, na yote aliyokuwa nayo."
➡️Naamini Sasa angalau kwa uchache umeelewa mambo yanayoweza kuletwa na Kiongozi wa familia, hivyo Baba au Mama wa familia ni Muhimu sana kumcha MUNGU katika KRISTO YESU ili usiwe chanzo Cha mabaya kwa Watoto wako na wajukuu zako.
◾Madhara yanayoweza kuletwa na kiongozi wa familia husika
1. MUNGU anaweza kuifuta baraka aliyowahi kuisema yeye juu ya familia hiyo kwa sababu ya kiongozi wa familia hiyo.
Mfano hai ni huu
1 Samweli 2:30 "Kwa sababu hiyo, BWANA, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa BWANA asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu."
➡️Hivyo kumdharau MUNGU Kwa Kiongozi wa familia kunaweza kusababisha MUNGU aifute baraka ya familia husika hata kama aliwahi kuitamka yeye MUNGU kwamba itakuwa yao.
◼️Kiongozi wa familia Hakikisha una YESU KRISTO na unaishi Maisha Matakatifu ili usababishe familia Yako ipate baraka na sio hasara.
2. Ukifanya mabaya sana kwa watu wengine mabaya hayatoondoka katika familia yako.
Mithali 17:13 "Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake."
➡️Hii ni Kanuni ya kiroho kwamba Kuna mabaya ukiwafanyia watu, mabaya hayo hayo hayataondoka kwenye familia Yako.
Mfano Unaweza kuwa muuaji na baadae Watoto wako au wajukuu zako wakajiua bila sababu za maana kumbe "mabaya uliyoyafanya hayataondoka nyumbani kwako"
3. Kufanya uongo ukimsingizia MUNGU atasababisha madhara kwa familia yako na wewe.
Mfano hai ni huu.
Yeremia 20:6 "Na wewe, Pashuri, na watu wote wanaokaa katika nyumba yako, mtakwenda utumwani; nawe utafika Babeli, na huko utakufa, na huko utazikwa, wewe, na rafiki zako wote, uliowatabiria maneno ya uongo."
◼️Huyu alitabiri uongo akimsingizia MUNGU maana Watabiri wengi husema wametuma na MUNGU, kilichofuata yeye kusababisha familia yake yote kwenda utumwani.
➡️Ndugu, usimhusishe MUNGU kwenye uongo wako usije kusababisha madhara kwa familia Yako
4. Kujitenga na MUNGU katika KRISTO YESU Kisha ukaanza kjabudu miungu au kuifanya familia yako iwe waabudu miungu utasababisha madhara mabaya zaidi kwa familia Yako.
1 Wafalme 21:22 "Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli."
➡️Yeroboamu alikuwa mwabudu miungu na alisababisha madhara makubwa kwa familia yake na Taifa Zima, hivyo wale wanaoabudu miungu hufananishwa na Yeroboamu na hupata madhara kama aliyoyapata yeroboamu.
Hivyo Kiongozi wa familia ukimwacha YESU KRISTO Kisha ukaanza kuabudu miungu utasababisha Madhara zaidi kwa kizazi chako na familia yako.
Na ukiwafundisha familia Yako kumwacha YESU ili waabudu shetani ndio kabisa hapo umewafanya wapotee na watapata madhara mabaya sana wakiwa Duniani na wasipopata Neema ya KRISTO utakuwa umesababisha familia Yako iende jehanamu.
◼️Mzazi Hakikisha familia Yako wote wanampokea Bwana YESU KRISTO kama Mwokozi wao ili wasipate madhara baadae.
5. Tabia za ajabu zitafuatana na watu wa familia yako wasimche MUNGU.
2 Samweli 12:11 "BWANA asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili."
➡️Ndugu kwa namna yeyote usiwe sehemu ya kuiletea madhara familia yako uliyoianzisha mwenyewe.
◾Nini ufanye juu ya familia yako ili kuleta mema na sio mabaya.
1. Usisababishe madhara ya umwagaji damu kwenye nyumba yako .
Kumbu 22:8 "Utakapojenga nyumba mpya, fanya ukuta kando-kando ya dari lako, usije ukaleta damu juu ya nyumba yako, mtu akianguka huko."
➡️Usiwe kama kaini aliyekosa makao yeye mwenyewe na familia yake baada ya kumwaga damu isiyo na hatia.
2. Tengeneza mambo ya nyumba yako ambayo hayako sawa mbele za MUNGU.
2 Wafalme 20:1 ''Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona."
3. Iweke familia yako baraka kwa utoaji mzuri mbele za MUNGU.
Ezekieli 44:30 "Na kitu cha kwanza cha malimbuko yote ya vitu vyote, na kila toleo la kila kitu
cha matoleo yenu, litakuwa la makuhani. Tena mtampa kuhani sehemu ya kwanza ya unga
mbichi, ili kukalisha baraka juu ya nyumba yako."
4. Hakikisha familia yako yote imempokea YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi na kuishi Maisha matakatifu.
Matendo 16:31 "Wakamwambia, Mwamini Bwana YESU, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako."
5. Ondoa miungu migeni katika familia yako ili umpendeza MUNGU wa Mbinguni.
Mwanzo 35:2 "Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu."
◼️Ndugu usiwe chanzo kwa namna yoyote kuleta madhara kwenye familia yako.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments