![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
➡️Mambo mengi yamekuwa hayaendi sana kwa watu wa MUNGU kwasababu "kutambua" imekuwa jambo ambalo halipo kwa baadhi ya watu.
◾Kutambua ni Nini?
◼️Kutambua ni kufahamu au kuelewa jambo.
➡️Wako watu wanaabudu na wachawi na hawajui.
➡️Unaweza ukapata madhara kwa sababu ya kutokutambua.
➡️Mfano ni huu, Kuna Watu walikuwa karibu sana na Elima mchawi na hawakujua kama ni Mchawi hadi alipokuja Paulo aliyekuwa na uwezo wa kutambua mtu wa ndani ya Mtu.
Matendo 13:6-11 " Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la MUNGU. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa ROHO MTAKATIFU, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za BWANA zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa BWANA u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza."
➡️Huyu Elima alikuwa mchawi ila alichinganyikana na watu wa MUNGU.
➡️Elima mchawi kazi yake mojawapo ni kuwatoa watu kwa YESU, ndio maana tunaona katika maandiko akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani ya Wokovu wa KRISTO, maana ndio kazi mojawapo ya roho za kichawi yaani kuwatoa watu kwa YESU.
◼️Paulo mwenye kutambua kwa sababu alikuwa na ROHO MTAKATIFU alipomtazama Elima alimuona akamtambua kiroho kwamba ana mambo 6 "akijaa ROHO MTAKATIFU, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za BWANA zilizonyoka?"
Yaani Elima alikuwa mchawi, Amejaa Hila , amejaa Uovu, ni Mtoto wa shetani yaani anamfuata shetani, ni adui wa Neno la KRISTO na anapotosha njia za MUNGU. Bila Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU Paulo asingeweza kuyaona hayo mambo 6 ndani ya Elima aliyekuwa ndani ya Kundi la watu wa MUNGU.
➡️Hata Leo akina Elima ni wengi sana.
➡️Ngoja nikupe mifano 2 hai.
Kuna rafiki yangu mmoja yeye na Mke wake ni wafanya kazi wa serikali, katika Maisha yao akatokea Mtumishi ambaye alianza kwa kuwaombea na baada ya muda mfupi sana akaanza kuwauliza "Nani Mwingine huwa anawaombea?" Wakanitaja Kisha Mtumishi yule Akawaambia kuanzia muda ule ni marufuku kuombewa na Mtumishi Mwingine yeyote Wala kuwa Karibu na Mtumishi Mwingine yeyote na mambo yao kiroho wasimshirikishe Mtu Mwingine yeyote, alipooana amefaulu katika hilo akaanza kuwadanganya kwamba Kuna Ufunuo juu yao, Ufunuo huo ulilenga kuuza vitu vyao vyote hadi vitanda na vyombo akisema wanatakiwa kuanza upya, wakauza Kila kitu wakampa kama Sadaka, na mishahara yao kwa muda walikuwa wakiipokea wanamkabidhi yeye kwa Mafundisho yake ya uongo, alipooana wameishiwa hawana Kila kitu, wameuza hadi viwanja na Hadi nguo zote akaondoka kwao yaani aliwapa hasara ya mamilioni.
Alipoondoka kwao na hawajapata msaada wa kiroho ndipo wakanipigia simu kunieleza, kukagua mitandaoni yule Mtu ni wakala wa shetani na ana tuhuma za kutapeli Maeneo mengi Tanzania .
Ndugu, Ukiwa na Roho ya kutambua Mtu kama huyo kabla ya uharibifu wake utakuwa unamjua.
Namshukuru MUNGU Kwa Neema yake miaka 3 iliyopita alinionyesha hadi mambo ya miaka 17 ijayo nikashangaa sana.
Katika KRISTO YESU Kuna kuona mambo yajayo.
Nakumbuka baada ya Kuokoka mwaka 2008 mwishoni niliendelea vizuri na Wokovu, miaka mwili baadae nilionyeshwa katika Maono mambo ya miaka zaidi ya kumi baadae, mengine yameshatimia kama nilivyoona na Moja bado muda wake wa kutumia ila najua lipo kama lilivyo.
Ndugu, katika KRISTO YESU Ukiwa na ROHO MTAKATIFU Kuna kuona na kutambua yajayo.
Yohana 16:13 "Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake."
➡️Mfano wa pili na kwanini ni Muhimu sana kuwa na macho ya rohoni ya kutambua.
Siku Moja nikiwa safarini nilikaa siti ambayo pembeni yangu alikuwa amekaa Dada mmoja Mrembo, rohoni mwangu nilijua Nini kinaendelea baada ya Ufunuo wa live, kumbe alikuwa Mhubiri , baadae kidogo yule Dada alianza kunishuhudia nihamie Kanisa lao akitoa sifa kwa mwanzilishi wa dhehebu lao na ambaye wao wanamuita mungu wa pili, wakati Dada yule akiendelea kuelezea dhehebu lao kwa ujasiri niliona Maono rohoni ya ajabu sana muda ule ule, niliambiwa Kanisa kile ni la kishetani na mkuu wa dhehebu lao ambao wao wanamuita Eliya eti kwamba alichukuliwa Mbinguni kwa gari la farasi wakimuiga Nabii Eliya wa kwenye Biblia, nilionyeshwa Eliya wao feki akiwa hayuko Mbinguni yaani hakwenda uzima wa Milele, nadhani unaelewa wasioenda uzima wa Milele huenda wapi.
Sasa kwa sababu Dada yule hakuwa Mtumishi wa Bwana YESU maana alikuwa wakala wa shetani ili anishawishi.
Mimi nilipata Neema ya kufunuliwa je wote amabayo aliwashawishi nje na Mimi walikuwa na Roho ya kutambua?
◼️Ndio maana nasisitiza unamhitaji sana ROHO MTAKATIFU ili uwe na uwezo wa kutambua.
➡️Leo Kuna hadi Watumishi wengi sana ni mawakala wa shetani na wamejiita majina ya Watakatifu wa Zamani Mfano kama huyo aliyejiita Eliya.
Watu hawa shetani amewapa kinywa Cha ushawishi na Wana kibali Cha kipepo kinachowavuta watu, wanachanganya ukweli na uongo kwa wakati mmoja.
Wana mapepo ya utambuzi hivyo anaweza akakuambia mambo Yako kwa usahihi kabisa Kisha akasema Makanisa yote hayana MUNGU hivyo mfuate yeye Kisha ukimfuata anaanza kukufundisha kwamba YESU haokoi, ROHO MTAKATIFU ilikuwa zamani na Mafundisho mengine ya uongo na hapo unajikuta umemwacha YESU.
Ndugu uwe makini sana na Hakikisha umeokoka na una ROHO MTAKATIFU.
◼️Leo omba MUNGU akupe neema ya kutambua.
➡️Kumbuka Kuna watu mwili wa nje ni kondoo ila ndani ni mbwa mwitu ukimtambua huyo hutafunga nae ndoa, hutashirikiana naye wala hutomweleza shida zako.
Watu hao unaishi nao, unashirikiana nao na wengi hata wanaweza kuwa ni ndugu zako.
Luka 10:3 "Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu."
➡️Usipowatambua unaweza kupata madhara au hasara.
Luka 19:44 "watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako."
◾Ufanye nini katika maombi
1. Tubia dhambi zako na kuziacha.
Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"
2. Omba kufumbuliwa macho yako ya rohoni.
➡️Mfano ni hawa walifumbuliwa macho kiroho wakamtambua Bwana YESU KRISTO.
Luka 24:31 "Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao."
3. Omba mtu wako wa rohoni awe na uwezo wa kutambua.
1 Wakorintho 2:15 "Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu."
✔️Kila Mtu ana utu wa aina 2, utu wa nje ndio huu unaoonekana ambao unatumia macho ya Kawaida kuona na utu wa rohoni ambao unaona kutokea ulimwengu wa roho Mfano kwa Maono, ndoto n.k
Huo utu wa rohoni Biblia pia inauita Mtu wa rohoni, hivyo muombee Mtu wako wa rohoni awe na uwezo wa kutambua.
4. Katika Jina la YESU KRISTO Pambana kimaombi na kila adui unayefunuliwa kutoka ulimwengu wa roho
Warumi 8:37 "Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments