MAOMBI YA KUOMBEA HATUA ZAKO ZA MAFANIKIO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.

Karibu Tujifunze Neno la MUNGU juu ya kuombea hatua zetu za kuelekea mambo mbalimbali mazuri au hatua za kupata baraka za MUNGU.


Ukisoma Yeremia 10:23 inaonyesha Kuna mambo ya Mwanadamu ni nje na uwezo wake kuyapata  hivyo anahitaji uwezeshaji wa MUNGU, Biblia inasema "Ee BWANA, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu."


◼️Njia ya mwanadamu haiku katika nafsi yake .


◼️Kuelekeza hatua za mwanadamu haiko katika uwezo wa mwanadamu hivyo hatua ya Kwenda kwenye kufanikiwa katika lolote jema unamhitaji MUNGU katika KRISTO YESU .


➡️Watu wa MUNGU tangu zamani waliombea hatua zao.


Zaburi 119:133 "Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki."


◼️Hata wewe Leo ombea hatua za kufanikiwa kitu fulani unachohitaji.


✔️Ili uifikie Ndoa au kupata kazi  unahitaji Hatua za kwenda hadi uifikie.


✔️Kila baraka ili kuipata inahitaji hatua.

Kuna hatua za kuelekea utajiri, Kuna hatua za kuelekea kuzaa au kupata kibali kibali kikubwa n.k


◾Hatua ni Nini?


➡️Hatua ni safari ya kuelekea kitu Fulani .


➡️Hatua ni mambo ambayo mtu anayafanya ili yamfikishe katika eneo alilokusudia.


➡️Kumbuka pia adui yaani mawakala wa shetani katika ulimwengu wa roho wanaweza kuvizia hatua za Mtu.


Maombolezo 4:18 "Wanatuvizia hatua zetu, Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu; Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia; Maana mwisho wetu umefika."


◾Sasa Kwanini tuombee hatua zetu?


1. Ili MUNGU aziongoze hatua zetu.


Mithali 16:9 "Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali BWANA huziongoza hatua zake."


2. Kuna adui kwenye ulimwengu wa roho anaweza kuvizia hatua zetu.


Maombolezo 4:18 "Wanatuvizia hatua zetu, Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu; Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia; Maana mwisho wetu umefika."


3. Ili MUNGU azifanyie nafasi hatua zako ili ufanikiwe.


2 Samweli 22:37 "Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Wala miguu yangu haikuteleza."


4. Kwa sababu mambo yote ili tufanikiwe tunatakiwa kuyafanya katika Bwana YESU KRISTO.

                             

Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

                    

5. Ni kwasababu  kuna hatua za mtu zinaweza kuelekea mauti na sio uzima.


1 Samweli 20:3 "Daudi akaapa, akasema, Baba yako anajua sana ya kuwa nimeona kibali machoni pako, naye asema, Yonathani asilijue neno hili, asije akahuzunika; lakini ni kweli, aishivyo BWANA, na iishivyo roho yako, iko hatua moja tu kati ya mimi na mauti."


◼️Sababu inayoweza kuzifanya hatua za Mtu kuelekea mauti au uharibifu ni hizi.

 

➡️sababu ni kufuata akili zake mwenyewe.


Warumi 1:28 "Na kama walivyokataa kuwa na MUNGU katika fahamu zao, MUNGU aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa."

     

➡️sababu  nyingine ni kulemewa na dhambi.


 Warumi 6:23 "Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu."


➡️sababu nyingine ni kuufata uongo wa shetani.


1 Timotheo 4:1 "Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;"

         

◾Mambo ya kujua kuhusu hatua za Mtu 


1. Hatua za mtu zinaweza kuhesabiwa .


Ayubu 14:16 "Lakini sasa wazihesabu hatua zangu; Je! Huchungulii dhambi yangu?"

            

2. Hatua za mtu zinaweza kuondoshwa .


Zaburi 17:5 "Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa."


3. Mambo yote unayohitaji yanahitaji hatua ili kuyafikia.


✔️Mimi Peter Mabula ngoja nikupe Mfano mmoja  Wewe rafiki yangu unayesoma somo langu ili na Wewe utafute mifano hai katika Maisha Yako.

Mfano ni huu wa kupata mwenzi wa Ndoa ambao unahitaji Hatua ili kufikia Ndoa.


Yeremia 29:6 "oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue."

   

4. Hatua za mtu zinaweza kuimarishwa na MUNGU .


Zaburi 37:23 "Hatua za mtu zaimarishwa na BWANA, Naye aipenda njia yake."


◾Nini ufanye katika Maombi.


1. Ombea hatua zako kiroho zisigeuke Kwenda kinyume na MUNGU.


Ayubu 31:7 "Kwamba hatua yangu imekengeuka na kuiacha njia, Na moyo wangu kuyaandama macho yangu, Tena kwamba kipaku cho chote kimeshikamana na mikono yangu;"

    

2. Kata hila za shetani juu ya hatua zako za mafanikio.


Zaburi 17:11 "Sasa wametuzunguka hatua zetu, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini."


3. Omba ROHO MTAKATIFU aongeze hatua zako.


Mithali 16:9 "Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali BWANA huziongoza hatua zake."


◼️MUNGU huziongoza hatua zetu kupitia ROHO MTAKATIFU.


 Yohana 16:13 "Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake."


4. Pambana na adui anayevizia hatua zako za mafanikio.


Maombolezo 4:18 "Wanatuvizia hatua zetu, Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu; Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia; Maana mwisho wetu umefika."


5. Kataa hatua zako kuondoshwa na adui.


Zaburi 17:5 "Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa."


6. Ombea hatua za kila jambo unalotaka ufanikiwe.


3 Yohana 1:2 "Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo."

                                   

7. Omba MUNGU aimarishe hatua za mafanikio.


Zaburi 37:23 "Hatua za mtu zaimarishwa na BWANA, Naye aipenda njia yake."


➡️Maombi ya kuanzia kwa wasio wazoefu wa kuomba Maombi ya muda mrefu, kwa wazoefu wa Maombi ninaamini walipoona somo waliandika points za kuomba na wataomba.


Maombi.


Baba yangu wa Mbinguni Jina lako litukuzwe.

Ninakushukuru kwa kunilinda na kunipa Neema mpya ndani ya KRISTO.


Niko mbele zako Baba ninaomba unisamehe dhambi zangu zote ninazozikumbuka na nilizozisahau.


Ee Bwana YESU KRISTO Mwokozi ninaomba ulifute Jina langu katika Kitabu Cha Hukumu na katika vitabu vya kuzimu vyote, na Sasa Bwana YESU uliandike Jina langu katika Kitabu chako Cha Uzima wa Milele.


Leo nimeamua kuanza na Wewe Bwana YESU  ili uwe Bwana na Mwokozi wangu.


Nakushukuru MUNGU Baba kwa kunisamehe dhambi zangu zote, makosa yangu yote na maovu yangu yote.


Kuanzia Sasa namkataa shetani na kazi zake zote, kuanzia Sasa naambatana na Bwana YESU ili awe  Mwokozi wangu Milele.


Nakushukuru Bwana YESU KRISTO kwa kuniokoa na kuliandika Jina langu katika Kitabu cha Uzima.


Sasa Baba wa Mbinguni Niko mbele zako nikiombea hatua zangu sawasawa na Neno lako nililojifunza Leo.

Nakusihi Mfalme wa Mbinguni imarisha hatua zangu za kuelekea Ndoa, kazi, biashara na kuelekea Kila baraka yangu iliyo katika Neno lako.


Nakusihi MUNGU wangu ponya hatua zangu ili nisielekee mabaya Bali nielekee mema yaliyo Yako.


Kwa Mamlaka ya Jina la YESU KRISTO ninaombea hatua zangu zote za kufanikiwa, Mimi natangaza katika Jina la YESU KRISTO nitafanikiwa katika hatua zangu za kupata kazi, kupata Ndoa, kupata Visa, kupata Watoto katika Ndoa, kupata uchumi mzuri na kupata Kila baraka yangu iliyo haki yangu.


Katika Jina la YESU KRISTO ninamfukuza Kila adui anayefuatilia hatua za kufanikiwa kwangu, katika Jina la YESU KRISTO adui toka na hutarudi Tena kuzuia hatua zangu.


Nitakushukuru MUNGU Baba maana katika Wewe nimeshinda.


Katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi nimeomba na ninapokea ushindi.

Amen Amen Ameeeeeeen.


 Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments