![]() |
| Na Mwl Peter Mabula na Jemimah Mabula Watenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU kuhusu maadui wa Ndoa.
◼️Moja ya kitu Muhimu sana kwenye Maisha ya Mwanadamu ni Ndoa.
◼️ Ndoa ni zawadi nzuri tuliyopewa na MUNGU duniani.
Kwa hiyo ni jukumu kwa kila Mteule wa KRISTO kuiheshimu ndoa yake.
Waebrania 13:4-5 " Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa."
◼️Upendo ni wa Muhimu sana katika Ndoa, Upendo sahihi ndio msingi wa ndoa.
◼️Kuaminiana ni jambo la muhimu sana katika Ndoa, Kuaminiana ni jukumu la wanandoa wote.
◼️Ndoa bila Wokovu hupitia mabaya mengi kwa sababu ya kukosekana kwa hofu ya MUNGU hivyo Wokovu wa KRISTO ni vazi la kudumu analotakiwa kulivaa kila mwanandoa siku zote.
◾Sasa Utajuaje kama umri wa Kuoa au kuolewa umefika?
◾Mambo 5 yanayoweza kukujulisha kwamba muda wako au Kuoa au kuolewa umefika.
1. Umri unaweza kukujulisha.
Mwanzo 29:18 "Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo."
◼️Yakobo tangu akiwa Mtoto Mdogo alikuwa na upendo kwa watu wengi ila hakuwa na upendo wa Ndoa, upendo wa Ndoa ulikuja kipindi Yakobo amefikia umri wa Kuoa, na upendo wa Yakobo wa Ndoa ukaangukia kwa Binti Rachel.
◼️Umri unaweza kuwa ni julisho ndani Yako kwamba ni muda wa kuoa au kuolewa kwa Binti.
◼️Wakati umri ukikujulisha kuhusu kuoa au kuolewa hata akili Yako na mawazo Yako yatakuwa tanawaza Ndoa na namna ya kuishi katika Ndoa Yako.
2. Watu kukujulisha.
Mwanzo 24:4 "bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke."
◼️Utajuaje kama umri wa kuingia katika Ndoa umefika?
Dalili ya pili kwamba muda wako wa kuingia katika Ndoa umefika ni watu wengine kukujulisha.
➡️Katika andiko tunaona Ibrahimu akimuagiza Eliazari Mtumishi wake aende katika nchi yao akamletee Mke Isaka, Nina uhakika Isaka anapoenda kuletewa Rebecca alikuwa na taarifa tayari, hivyo Ibrahimu alikuwa amemwambia juu ya muda wake wa kuoa umefika.
Hivyo hata kwako Kaka au Dada kama hujui kama muda wako wa kuingia katika Ndoa umefika MUNGU anaweza kutumia watu kukujulisha.
Utasikia "Oa Sasa", "ni wakati wako olewa Sasa", "unasubiri Nini Kuoa/Kuolewa", "Changamka tunataka kula ubwabwa" n.k
3. Mazingira kukujulisha.
Yeremia 29:6 "oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue."
➡️Biblia inasema "oeni" Tena Biblia inasema "Kawaozeni Binti zenu"
Hii Ina maana Kijana kuoa au Binti kuolewa jambo hilo la Ndoa limefungwa kwenye muda, muda huo ukifika mazingira tu yatakujulisha unahitaji kuingia kwenye Ndoa.
◼️Wakati huo utatamani Ndoa kuliko chochote.
◼️Utaona upweke kukaa bila kuoa au kuolewa, utaona ni vizuri zaidi kwako kuwa katika Ndoa n.k
◼️Utaona jambo zaidi kwako wakati huo ni kuwa na mwenzi wa Ndoa ili mzae Watoto na muwe na familia yenu nzuri.
◼️Mazingira tu yanaweza kukujulisha kwamba Sasa unatakiwa Kuoa au kuolewa.
4. Kufunuliwa hilo kwa maombi.
Mathayo 1:20 "Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa BWANA alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa ROHO MTAKATIFU."
Mimi Peter Mabula ninachotaka uone rafiki yangu ni hiki "malaika wa BWANA alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo" maana yake katika ndoto Yusufu alifunuliwa kwamba Mariamu ndio Mke mwema wake.
◼️Kwa Ufunuo wa MUNGU unaweza kujulishwa juu ya muda wa kuingia katika Ndoa na nani wa kuingia naye katika Ndoa.
◼️Kuna watu baada ya Maombi katika jina la YESU KRISTO wanaota ndoto, wanaona Maono au wanasikia Sauti ya ndani juu ya Ndoa, hiyo maana yake wakati umefika hivyo fanyia kazi jambo hilo la Ndoa.
Mazingira hayo ya kufunuliwa ndio yatakuunganisha na Muujiza wako wa Ndoa kama ukifanyia kazi.
5. Shauku inayoendana na malengo ya kuingia kwenye ndoa. Na malengo hayo yawe na mipango mizuri.
Mwanzo 34:4 "Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu."
➡️Katika andiko hili ni shekemu mpagani aliyetaka kumuoa Mtumishi wa MUNGU Dina, kitu ambacho kiroho hakitakiwi kuwezekana, ndio maana haikuwezekana, pia shekemu alitumia njia ya dhambi kupata Ndoa, ndio maana haikuwezekana.
➡️Ninachotaka uone hapa sio kushindwa kwa shekemu ila ninachotaka uone ni shauku yake ya kupata Ndoa, shauku kama hiyo haiji Kila Wakati Bali huja wakati sahihi
➡️Hata kwako unaweza ukashangaa mwaka fulani shauku na kuoa au kuolewa ni kubwa sana sana, hilo ni julisho kwako kwamba muda sahihi wa kuingia katika Ndoa umefika.
➡️Baada ya kukueleza mambo hayo 5 yatakayokujulisha kwamba muda wako sahihi wa kuingia katika Ndoa, ngoja niseme pia ushauri huu kwako unayetarajia Ndoa.
◼️ Haijalishi una shauku ya Ndoa ndani Yako, haijalishi mazingira yanakutaka uoe au uolewe, haijalishi umri wako wa Ndoa umefika, haijalishi ni Nini ila usije kamwe ukaingia kwenye Ndoa ni Mtu mpagani yaani Mtu ambaye hajaokolewa na Bwana YESU KRISTO.
Biblia inakataza kuunganishwa na watu wasiomwamini YESU KRISTO kama Mwokozi wao.
2 Wakorintho 6:14 "Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?'
◼️Ukiingia katika Ndoa na Mtu asiye na YESU KRISTO ni kwa hasara Yako na hasara ya kizazi chako wasipopata Neema.
➡️Mfano hai Suleiman alijua Kanuni hii kwamba Mteule wa MUNGU hatakiwi kuingia katika Ndoa na mwabudu miungu.
1 Wafalme 11:2 "na wa mataifa BWANA aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda."
Matokeo ya kuoa mpagani yalikuwa mabaya, Biblia inasema katika 1 Wafalme 11:4 kwamba "Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake."
➡️Wapagani hawa walimgeuza Moyo Mtumishi wa MUNGU akaanza kufuata miungu, ni mbaya sana.
◼️ Ukiingia katika Ndoa na Mtu wa dini nyingine nje na KRISTO ni zaidi ya kuingia katika Ndoa na mpagani.
Kumbu 7:3-4 " binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya BWANA juu yenu, naye atakuangamiza upesi."
◼️Hivyo zingatia sana kuingia katika Ndoa na Mtu aliyeokoka hata kama anatokea nje na dhehebu lako maana huyo aliye na YESU KRISTO ni mrithi pamoja na Wewe wa uzima wa Milele.
1 Petro 3:7 "Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe."
◾Yote kwa yote ni muhimu sana kujua kwamba ili ufanikiwe katika baraka hii ya Ndoa unahitaji mambo matatu.
1. Maisha matakatifu ya Wokovu.
1 Petro 1:14-15 " Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"
2. Uchaguzi sahihi unaotokana na maombi sahihi.
Wagalatia 5:16" Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."
3. Kuyajua majira sahihi ya wakati wa MUNGU juu ya baraka hiyo.
Yohana 16:13" Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments