![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Najua yamkini Wewe ni mtoaji mzuri wa Sadaka na Zaka, unafanya vyema sana maana Sadaka njema Zina kazi pia kubwa kwa ajili Yako katika ulimwengu wa roho, hata MUNGU anaweza kuzikumbuka na kukutimizia mahitaji Yako yote.
Zaburi 20:3-4 " Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote."
➡️Biblia inaposema "Mahitaji Yako yote" Ina maana hata yale mahitaji magumu sana kwako MUNGU anaweza kukutimizia kwa sababu tu ya utoaji wako matoleo wa uaminifu mbele zake.
✔️Vipi kama hilo la "mahitaji Yako yote" kwako ikawa ni kupona ugonjwa mbaya ambao madaktari wamesema huwezi kupona?
✔️Vipi kama hiyo "Mahitaji Yako yote" kwako ikawa ni ulinzi wa MUNGU sehemu ambayo umezungukwa na mawakala wa shetani wengi na wenye Nguvu?
◼️Biblia inaposema "Mahitaji Yako yote" ni hakika ni Kila hitaji lako gumu sana linaweza kubadilika na kuwa Muujiza wa MUNGU ukakufuata.
➡️Yamkini Wewe hutoa Zaka na Sadaka ila mara Moja Moja.
➡️ Labda Wewe ni yule ambaye uko busy kulaani utoaji wa Zaka na Sadaka kwa sababu ya chuki zako kwa Watumishi wa MUNGU wanaopokea Sadaka.
Mimi Peter Mabula Niko hapa kukuambia rafiki yangu unayesoma somo langu hili kwamba Kuna watu Maisha yao yalibadilishwa na Sadaka, Kuna hadi watu hawakufa mbele ya adui zao kwa sababu sadaka zao zilikumbukwa mbele za MUNGU wakalindwa ili waendelee kuwa Mfano kwa jamii juu ya uaminifu wao kumtolea MUNGU wa Mbinguni Zaka na Sadaka njema, kwenye maandiko Kuna hadi watu walifufuka kwa sababu Sadaka zao zilizungumza.
◼️Ndugu, kwa MUNGU wa Mbinguni hakuna kitu Cha Hasara kama unafanya katika yeye kwa njia ya YESU KRISTO ndani ya Wokovu wake.
Matendo 10:31 "akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za MUNGU."
◼️Sadaka zinaweza hata kuwa chanzo Cha Ufunuo wenye msaada kwa mtoaji.
◼️Ngoja nikuletee watu 4 ambao Sadaka zao mbele za MUNGU zilibadilisha hatima zao na Maisha yao.
◾Watu 4 ambao Maisha yao yalibadilishwa na Sadaka zao.
1. Dorkasi Alikufa akafufuka kwa sababu ya Sadaka zake.
Matendo 9:36-42 " Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini BWANA."
◼️Huyu hatima yake ilikuwa ni kifo lakini utoaji wake ukaileta hatima ya kuishi Tena, Ndugu usidharau Sadaka unazomtolea MUNGU wa Mbinguni katika KRISTO YESU Kwa uaminifu na Maisha ya haki.
◼️ Ndugu, Kuna mazingira mengine hata Maombi ya Watumishi hayatumii Nguvu nyingi kwa sababu kwa Mtu wanayemuombea Kuna kitu kingine kinazungumza katika ulimwengu wa roho ambacho ni Sadaka njema alizomtolea MUNGU huyo Mtu.
◼️ Ndugu Hakikisha MUNGU akikubariki usimsahau kumtolea Zaka na Sadaka maana huo ni utoaji ni kwa faida Yako.
Matendo 20:35 "Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana YESU, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea."
2. Ibrahimu alipandishwa viwango kiroho na kubarikiwa baada ya utii wa wito wa Sadaka.
Mwanzo 22:15-18 " Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu."
➡️Hapo tunaona hatima ya Ibrahimu inakuwa kubwa sana baada ya utii wa kumtolea MUNGU Sadaka ambayo MUNGU amemwambia.
➡️Utoaji wa Ibrahimu usio na Kona Kona Wala usio na ubabaishaji ulisababisha MUNGU aape jambo zuri sana kwa Ibrahimu kwamba atambariki na kumfanya yeye awe chanzo Cha baraka kwa wengine.
➡️Je Wewe uliposikia msukumo moyoni Mwako wa kumtolea Bwana YESU Sadaka au Zaka au Dhabihu ulitii?
Mwenzako Ibrahimu baada tu ya kutii Kuna kitu kikaongezeka kwenye Maisha yake, na Kuna sehemu hadi Bila inasema kwamba " Kila atakayemlaani Ibrahimu atakuwa amelaaniwa na MUNGU"
Mwanzo 12:3 "nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa."
➡️Hivyo Ukitaka upokee laana ya lazima basi mlaani Ibrahimu mtoa sadaka ya ajabu na ambaye ana Mcha MUNGU wa Mbinguni.
◼️Ndio maana Biblia Kwa maneno machache tu inakutaka usimsahau MUNGU kupitia Mali zako maana faida kwako ni nyingi yaani kwa maana nyingine mheshimu MUNGU Kwa Mali zako.
Mithali 3:9-10 " Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya."
3. Kornelio alipata neema kubwa iliyotokana na usafi na Sadaka .
Matendo 10:1-4 " Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa MUNGU, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba MUNGU daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa MUNGU, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za MUNGU."
◼️Hata wewe unaweza ukapata Neema kwa sababu tu ya utoaji wako unaoambatana na kumcha MUNGU katika KRISTO YESU.
◼️Sadaka zako zinaweza kuwa ukumbusho mbele za MUNGU hivyo zinaweza kusababisha jambo jema kwako maana zinaonekana.
◼️ Ndugu, usije ukanidharau Sadaka unazomtolea MUNGU wa Mbinguni.
◼️ Ndugu usije ukanidharau Fungu la kumi au kwa Jina lingine Zaka unazomtolea MUNGU wa Mbinguni, hizo zinaweza kuleta Neema ya ajabu Maishani Mwako.
4. Nuhu baada ya Sadaka yake tangazo la Mbinguni likatolewa kwamba nchi haitolaaniwa tena.
Mwanzo 8:20-22 " Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma."
◼️Sadaka njema kwa MUNGU zinaweza kubadilisha Maisha ya Mtu husika na hata jamii nzima, baada ya Sadaka ya Nuhu tangazo la ajabu lilitoka kwamba gharika ya kuua Dunia nzima haitatokea Tena.
◼️Ndugu, usiache kumtolea MUNGU Sadaka na Zaka maana kwa njia hiyo pia unamtumikia MUNGU wa Mbinguni, Kuna muda wa kuvuna kama hutazimia Moyo.
1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."
◼️Zingatia toa Sadaka zako na Zaka zako kwa Mtumishi ambaye ameokoka, anaishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa KRISTO na awe na ROHO MTAKATIFU ndani yake.
Waisraeli waliambiwa wasitoe Matoleo yao Kila wapaonapo ila kule ambako MUNGU yupo.
Kumbu 12:5-6 " Lakini mahali atakapochagua BWANA, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko; pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo;"
◼️Hata wewe Ndugu toa Matoleo Yako kwa Mtumishi ambaye una uhakika anamtumikia Bwana YESU KRISTO na sio vinginevyo.
◼️Toa pia kwa Moyo wa kumpenda MUNGU.
2 Wakorintho 9:7-8 " Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na MUNGU aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;"
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments