KUFAHAMU MAANA YA NENO ''NAKUPENDA''

1Wakorintho 13:4-6{Upendo …haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli.}

SAMWEL MABULA NA MKEWE HAPPY MASAWE BAADA YA KUFUNGA NDOA
Neno KUPENDA, au UPENDO, limekuwa msamiati mgumu sana kwa vijana wa leo, shetani amefanikiwa kwa asilimia 90 kuwanasa vijana wengi na kuwaangusha katika dhambi, akitumia msamiati huu NAKUPENDA. Nikiwa katika huduma zangu za Injili, nilikutana na binti mmoja ambaye alikuwa amezidiwa kitandani akiwa anaumwa, lakini pia alikuwa mja mzito. Nilipomuuliza mumewe yuko wapi, akaanza kulia, mwishowe akaeleza kisa cha kusikitisha jinsi kijana wa kiume alivyomdanganya kuwa anampenda, lakini baada kutimiza haja yake, akampiga “KIBUTI” hakutaka hata kumuona, alitelekezwa bila msaada. Vijana wengi leo hasa wa kike wanaingizwa “CHAKA” wanadanganywa na vijana wa kiume kwa neno NAKUPENDA, Binti akiambiwa nakupenda, utamuona Macho na masikio yanaaza kulege, kusema ukweli wengi HAWAPENDI, bali WANATAMANI. Wengi wamepitia changamoto hiyo ya kuambiwa wanapendwa, lakini baadaye walijikuta hukana Upendo. Na matatizo ya ndoa nyingi za siku hizi yanatokana na mwanzo wa mahusiano kuwa ni kukidhi TAMAA ya mwili. Misukumo na Mihemuko ya Tamaa za NGONO imechukuliwa na Vijana wengi kuwa ni Upendo. Utakuta kijana wa kiume anaonyesha hisia zote za kupenda, yuko tayari kukupigia magoti, kukulamba miguu, kukupatia chochote utakacho, ili mradi akuonyeshe kuwa anakupenda. Kisa cha Amnoni na Tamari katika biblia “1Samweli 13:1-22”, kinaeleza jinsi Amnoni alivyougua kwa kumpenda dada yake Tamari, lakini baada ya Kuzini naye, Mihemuko ya Ngono ilipoisha akamchukia Vibaya sana.
Kuna ujinga ambao shetani ameuhalalisha kwa vijana wa kizazi hiki, kuwa Upendo unadhihirishwa kwa tendo la NGONO, yaani bila kumuonjesha eti utakuwa hujakubali penzi lake, na wengine ukiwanyima eti wanaangua kilio nakusema “Darling mwenzio utaniua aaaaaa” , Mwambie kama kweli unanipenda basi kufa nione, utashangaa macho makavuu! anaendelea kula dagaa. KIJANA ANAYELILIA NGONO KABLA YA NDOA HAKUPENDI ANAKUTAMANI, na jambo la hatari kabisa ni kwamba anakutenganisha na Mungu wako kwa kukuingiza katika Dhambi – Neno linasema “Enyi Wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa Dunia ni kuwa ADUI wa Mungu? …” Yakobo 4:4. Iweni na akili, upendo unaokutenga na Mungu wako una faida gani? Ulimwengu utakapokugeuka na Tufani kuvuma juu yako, utamkimbilia nani kama sio Mungu?
Wito wangu kwa vijana wote wanaopenda kuwa na maisha yenye Baraka za mungu ni huu “Basi Mtiini Mungu, Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu naye atawakaribia ninyi ….” Yakobo 4:7-8. Mungu anahitaji vijana wanaoweza kumwambia Shetani “NO” au “HAPANA”, mpaka lini Shetani ataendelea kutawala maisha ya vijana? It is time to say “NO” and be ready because JESUS is around the corner. Mwisho nawapongeza vijana wote waliotangaza NIA ya kufunga Ndoa halali, na kuachana na Dhambi ya Uzinzi. Nitazidi kuwaombea ili Mungu azidi kuifanikisha mipango yenu. MUNGU AKUBARIKI . 

Comments

Anonymous said…
Barikiwa sana mtumishi kwa Neno la uzima